Lango la habari, Simiyu
Kafulila amechukua uamuzi huo Alhamisi Mei 06, 2022 wakati wa kikao cha mafunzo ya usimamizi wa ununuzi wa pamba msimu huu kilichofanyika wilayani Bariadi mkoani humo.
Amesema maofisa na viongozi wa AMCOS wameshindwa kusimamia majukumu yao ipasavyo hivyo ni vema wakapisha sura mpya ambazo zitaendana na kasi ya mkoa.
"Inafahamika Simiyu ndio Simba wa Pamba Tanzania ikizalisha wastani wa asilimia 40 hadi 60. Pamoja na bei nzuri msimu uliopita kufikia Sh.1800, bado kuna malalamiko mengi yaliyothibitika mchezo mchafu kati ya AMCOS na Maofisa Ushirika uliosababisha mkulima kutopata bei halisi iliyolipwa na mnunuzi" alisisitiza RC Kafulila.
Aidha Kafulila amesema pamoja na kuwasimamisha kazi maofisa ushirika watano na kuvunja uongozi wa AMCOS, pia ameitaka PCCB kufanya uchunguzi imkuhakiki kila AMCOS ili kuona vielelezo na kuthibitisha malipo aliyolipwa mkulima na kiasi ambacho AMCOS iliuza pamba kwa niaba ya mkulima.
Amesema mpaka sasa zimechunguzwa AMCOS 189 na zote hakuna vielelezo kuthibitisha malipo sahihi kwa mkulima.
RC Kafulila amesema kwa kuzingatia changamoto hizo na zaidi maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kutaka kusafisha mfumo mzima wa usimamizi zao la pamba hasa katika msimu huu ambao makadirio ya Bodi ya Pamba yanaonesha Simiyu itavuna zaidi ya mara tatu ya msimu uliokwisha kwa kupata kati ya tani 250,000 mpaka 300,000.
Amesema kiasi hicho cha Pamba kinachotarajiwa kuvunwa hakijawahi kupatikana hata ukiunganisha na Mkoa wa Shinyanga.
Kafulila ameeleza mwelekeo mpya wa usimamizi wa manunuzi ya Pamba msimu huu unaonza Mei 20, 2022 ni kui imarisha uwajibikaji wa AMCOS kwa kuhakikisha AMCOS zote zinafutwa na hivyo uchaguzi utarudiwa ndani ya wiki Moja.
"Pili, ili kuhakikisha uchaguzi huo unaleta viongozi thabiti, wakulima wote wa pamba kwenye kijiji husika watakuwa na haki ya kushiriki uchaguzi. Hii inatokana na ukweli kuwa wanachama wa AMCOS hawazidi asilimia 30 ya wakulima wote.
Hivyo asilimia 70 ya wakulima ambao sio wanachama wa AMCOS washiriki uchaguzi huo. Haki hii pia inachangiwa na ukweli kwamba AMCOS zinalipwa shilingi kwa kila kilo ya Pamba bila kujali ni ya mwanachama au asiye mwanachama wa ushirika.
Mkuu wa mkoa huo alisema, ili kuongeza uwazi, wakati wa manunuzi msimu huu unaoanza Mei 20, 2022, kila AMCOS itapaswa kuweka wazi kwenye kituo cha manunuzi bei ya kila mnunuzi aliyewapa pesa wamnunulie pamba, ili wanunuzi watakaonunua pamba kupitia AMCOS wajue kwanini wanapata au wanakosa kulingana na bei zao wanazotaka AMCOS iwanunulie pamba.
"Nne, ili kuhakikisha usimamizi thabiti, Kafulila amelekeza wakurugenzi Halmashauri Bariadi Mjini, Vijijini, Maswa, Busega, Itilima na Meatu kuwaondoa maofisa ushirika wote ngazi ya wilaya na kupangiwa kazi zingine na taratibu za kuweka maofisa wengine zifanyike ndani ya wiki moja.
Tano, ili kuongeza uwazi na ushindani wanunuzi binafsi wataruhusiwa kuweka mawakala wao kwenye soko la pamba na kushindana na AMCOS katika masoko hayo vijijini na wote AMCOS na mawakala wanunuzi watasimamiwa na Serikali ya kijiji chini ya mtendaji wa kijiji,"amesema.
Amesema mtendaji wa kijiji ndio msimamizi mkuu wa uuzaji wa pamba akishirikiana na AMCOS.
RC Kafulila amesema jambo la sita, ili kuhakikisha usimamizi thabiti, pamba yoyote halali itapaswa kuwa na iliyouzwa kwa bei sawa au zaidi ya bei elekezi na iwe na kibali kilichothibitishwa na mtendaji wa kijiji na AMCOS pamba iliponunuliwa
Aidha, Kafulila amesema ili kuongeza ufanisi makatibu wa AMCOS watapaswa kutoka ndani ya kata husika.
Kwa upande mwingine amesema mkulima atakuwa na uhuru wa kuuza Pamba kwa AMCOS au wakala wa mnunuzi binafsi ambao wote watakuwa kwenye soko la pamba chini ya mtendaji wa kijiji.
"Tisa, wanunuzi wa Pamba watakuwa na uhuru wa kununua pamba kupitia AMCOS au wakala wake lakini manunuzi yote yatasimamiwa na Serikali ya kijiji. Wote, AMCOS na wakala wa mnunuzi watanunua Pamba kwenye soko ndani ya kijiji na VEO atakuwa na msimamizi mkuu,"amesema.
Kafulila amesema anawatakia wakulima na wananchi wote kutoa ushirikiano hasa ikizingatiwa kuwa usimamizi thabiti wa Serikali utaendelea kuhakikisha mkulima anapata bei nzuri.
"Nimeshiriki kikao cha wataalamu wa Bodi ya pamba, Ushirika na Wanunuzi wa pamba msimu huu kwa lengo la kuhakikisha mkulima anapata bei inayofanana na jasho lake. Najua Waziri atatangaza bei elekezi Mei 20, lakini nachoweza kuwahikishia wakulima ni kwamba bei itakuwa nzuri kuliko miaka yote katika kumbukumbu za pamba tangu mwaka 1990," alihitimisha ndugu Kafulila.
Mwisho