Na Said Muhibu, Lango La Habari
Rais wa Umoja wa Falme za kiarabu (UAE) Sheikh Khalifa bin Zayed Al-Nahyan amefariki dunia akiwa na miaka 73 kufuatia ugonjwa wa kiharusi aliokuwa anaugua tangu mwaka 2014.
Ripoti iliyotolewa na shirika la habari la Emirati state WAM imesema kuwa, Sheikh Khalifa amefariki dunia Mei 13 2022 leo ijumaa akiwa na miaka 73, bendera zitapepea nusu mlingoti na kufuatiwa na maombolezo rasmi ya siku arobaini pamoja na kufungwa kwa wizara na mashirika rasmi ya kiserikali na binafsi kwa siku tatu
"Wizara ya masuala ya urais ilitangaza kuwa kutakuwa na maombolezo rasmi ya siku arobaini, bendera nusu mlingoti na kufungwa kwa wizara na mashirika rasmi katika ngazi ya shirikisho na serikali za mitaa na sekta binafsi," shirika la habari Emirati state WAM liliandika kwenye ukurasa wa Twitter.
Sheikh Khalifa alionekana hadharani mara chache tangu alipopatwa na kiharusi mwaka 2014, huku kaka yake, Mwanamfalme wa Abu Dhabi, Mohammed bin Zayed akionekana kama mtawala mkuu na mtoa maamuzi wa maamuzi makubwa ya sera za kigeni kama vile, kujiunga na vita vinavyoongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen na kuongoza vikwazo kwa nchi jirani ya Qatar katika miaka ya hivi karibuni.
Sheikh Khalifa aliingia madarakani mwaka 2004 katika milki tajiri zaidi ya Abu Dhabi na kuwa mkuu wa nchi. Anatarajiwa kurithiwa kama mtawala wa Abu Dhabi na Mwanamfalme Sheikh Mohammed.