Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam limewakamata Vijana 31 wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu maarufu Panya Road kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya uporaji baada ya kuvunja nyumba, kujeruhi na kuiba vitu mbalimbali vya nyumbani.
Akithibitisha hilo Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ACP Jumanne Muliro amesema kuwa watuhumiwa hao wamekamatwa jana Alhamisi Mei 06, 22 ikiwa ni matokeo ya operesheni maalum kali na msako wa mtaa kwa mtaa dhidi ya Vijana wanaojihusisha na Makundi ya Panya Road.
Kamanda Muliro amesema kuwa operesheni hiyo ambayo ni endelevu ilianza April 27, 2022 na imefanikiwa kuwakamata Wahalifu hao ambao wengi wao ni vijana wenye umri kati ya miaka 13-20 na wakati wanafanya uhalifu wanatumia mapanga, visu, nondo, na mikasi mikubwa.
Amesema watuhumiwa hao walifanyiwa mahojiano ya kina ambapo walibainika kuhusika katika vitendo vya kihalifu na kuonesha baadhi ya vitu walivyoiba zikiwemo TV 12 na simu 4 za mkononi.
Aidha Kamanda Murilo ametoa onyo kali na kueleza kuwa Jeshi la Polisi halitasita kuwakamata ambao wamekuwa wakipokea mali mbalimbali za wizi zinazotokana na matukio ya kihalifu.
"Jeshi la Polisi halitasita kuwafikisha kwenye vyombo vingine vya kisheria wanaoshirikiana na wahalifu" amesema Kamanda Muliro