Na Said Muhibu, Lango la habari
Mwanajeshi wa Urusi mwenye umri wa miaka 21 anayejulikana kama Vadim Shishimarin amekiri kosa la kumuua raia wa kawaida katika mzozo unaoendelea baina ya Urusi na Ukraine, hii inakuwa ni kesi ya kwanza ya uhalifu wa kivita nchini Ukraine tangu mzozo baina ya nchi hizo kuanza.
Shishimarin alikiri kumpiga risasi ya kichwa raia wa Ukraine mwenye umri wa miaka 62 siku chache baada ya uvamizi wa Urusi kwa Ukraine. Kwa mujibu wa waendesha mashtaka Shishimarin aliamriwa kumuua raia huyon kwa kutumia bunduki aina ya Kalashnikov.
Mhalifu huyo aliletwa katika chumba kidogo cha mahakama cha kyiv leo hii, akiwa amefungwa pingu na kuzingirwa na walinzi waliobeba silaha nzito. Kesi ya Shishimarin iliahirishwa muda mfupi baada kukiri kwa tukio hilo na kusikilizwa tena Alhamis katika chumba kikubwa cha mahakama.
Mwendesha mashtaka mkuu wa Ukraine Iryna Venediktova alinukuliwa akisema kwenye mitandao ya kijamii ya kwamba, wale wote waliohusika kwa namna moja ama nyengine katika vitendo vya uhalifu wa kivita watawajibika.
“kwa kesi hii ya kwanza, tunatuma ishara wazi kwamba kila mhalifu, kila mtu ambaye aliamuru au kusaidia katika kutendeka kwa uhalifu nchini Ukraine hatakwepa kuwajibika,” aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.
Kwa upande wake Moscow imekanusha kuwa wanajeshi wake kuhusika na vitendo hivyo, ijapokuwa wachunguzi wamekuwa wakikusanya ushahidi wa uhalifu wa kivita unaoweza kufikishwa katika mahakama ya kimataifa inayoshughulikia masuala ya vitendo vya uhalifu wa kivita ICC The Hague.