Baraza Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema limeunga mkono uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho wa kuwafukuza uanachama Halima Mdee na wenzake 18 kwa kukubali kwenda kuapishwa na kuwa wabunge wa viti maalumu bila kupata baraka za chama hicho.
Maamuzi hayo yamefikiwa usiku huu Mei 12,2022 kwenye kikao cha Baraza Kuu kilichoanza kufanyika Mei 11,2022 katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam lenye ajenda tano na kuhudhuriwa na wajumbe zaidi ya 400 wa chama hicho, wanaotoka katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Katika maamuzi hayo Jumla ya kura 423 zilipigwa ambapo Kura 413 (97.6%) zimekubali uamuzi wa kamati kuu wa kuwafukuza wakina Halima Mdee na wenzake huku kura 5 (1.2%) zikitakata wasamehewe na kura 5 (1.2%) zikiwa hazifungamani na upande wowote.