Seveline Mbullu Na Samir Salum, Lango la habari
Mbunge wa Jimbo la Igunga Nicholaus Ngassa amewataka Viongozi wa Vyama vya ushirika kutunza skimu ya umwagiliaji inayosaidia katika kilimo hali inayokuza uchumi wa wananchi.
Mbunge Ngassa ametoa agizo hilo alipofanya ziara kwenye mashamba ya mpunga kwenye Skimu ya Mwamapuli iliyopo Mwanzugi Igunga kwa ajili ya kuona hali na mwenendo wa uzalishaji wa mpunga.
Amesema Kuwa Serikali ina agenda 10 hadi 30 yenye mikakati ya kuhakikisha inakuza kilimo kwa zaidi ya asilimia Kumi ifikapo Mwaka 2030.
Amesema moja ya mkakati wa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ni kuwa na kilimo cha umwagiliaji hivyo kuwataka viongozi wa chama cha ushirika kutunza skimu hiyo
"Sisi Igunga tumebahatika kuwa na Skimu kubwa ya umwagiliaji na inatoa mpunga kwa wingi, niwaombe Viongozi wangu wa ushirika tuitunze Skimu hii kwani ndio uti wa mgongo kwenye uchumi wa Wana Igunga wengi" Amesema Mh. Ngassa
Ameongeza kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto ya Mbolea kutokana na UVIKO 19 na Vita ya Urusi na Ukraine Serikali imejipanga kuhakikisha msimu ujao Wakulima wanapata mbolea kwa bei nafuu.
Aidha Mhe. Ngassa ametembelea vikundi mbalimbali vya wakulima na wafugaji kwa ajili ya kubadilisha mawazo juu ya uzalishaji wa kisasa wenye tija.