Breaking

Sunday, 8 May 2022

MACHIFU NA VIONGOZI WA KIMILA WATAKIWA KUSHAWISHI JAMII ZAI KUSHIRIKI SENSA





Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa ametoa wito kwa Machifu wote nchini na Viongozi wa Kimila kuhakikisha wanashawishi jamii zao kushiriki zoezi la kitaifa la sensa ya sita ya watu itakayofanyika Agosti 23, 2022.

Waziri Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Mei 7, 2022 kwenye ufunguzi wa mkutano wa Machifu na Viongozi wa Kimila kutoka mikoa yote hapa nchini uliofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salam.


Amesema Serikali inatambua mchango mkubwa wa viongozi hao na kwamba itaendelea kuwaheshimu, kuwajali na kuwasikiliza viongozi ili kuweza kujifunza mambo kupitia kwao ambapo amesisitiza kwamba mtu yoyote atakayejaribu kuwadharau viongozi hao atachukuliwa hatua.

Sisi watanzania hasa vijana wa karne ya leo, tuna mengi ya kujifunza kutoka kwenu kwani msingi wa mila ndio msingi wa maisha yetu, hatuwezi kuwa na maisha bora, amani wala utulivu kama hatutajikita katika misingi ya kimila na desturi za mtanzania” Ameendelea kufafanua Mhe. Mchengerwa

Awali akizungumzia sababu za serikali kufanya sense ya watu na makazi kila baada ya miaka 10 Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Tanzania Bara na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Anna Semamba Makinda, amesema Sensa inaisadia Serikali kufanya tathimini ya maendeleo ya taifa kwa kujua idadi ya watu, umri, jinsi na hali ya watu wake katika nchi.


Mama Makinda ameongeza kuwa Serikali inawachukulia viongozi hao kuwa ni kundi muhimu kwenye taifa letu kwa kuwa lina sikikiliza na jamii zote na lina ushawishi mkubwa kwa jamii zao hivyo litasaidia kufanikisha zoezi la sensa ya watu hapa nchini kwa kiwango cha juu.


Nyinyi mnaaminika zaidi kuliko yeyote katika maeneo yenu ya utawala, na tunaamini nyinyi mkisema hakuna atakaye wabishia, hamasisheni wananchi wote kuhesabiwa” amesisitiza Kamisaa Makinda.



Baadhi ya machifu walioshiriki semina hiyo akiwemo chifu Aisack Meijo ambaye ni chifu Mkuu wa Waamasai kutoka Monduli Arusha amempongeza Waziri Mchengerwa pamoja na wasaidizi wake kwa namna ambayo Wizara imekuwa akitoa ushirikiano kwa masuala ya kichifu kwa kuwa hudumia kwa wakati wahitaji na kutoa msaada pale inapohitaji.


Naye Chifu Michal Kayamba ambaye ni chifu wa kabila la Wakonongo kutoka wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi amesema hatua zinazochukuliwa na Serikali ya awamu ya sita katika kuitangaza Tanzania pamoja na tamaduni zake hazijapata kushuhudiwa katika kipindi kilichopita.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages