Breaking

Sunday, 8 May 2022

WANANCHI WAASWA KUJENGA UTAMADUNI WA KUZUNGUMZA MASUALA YA KIFAMILIA KUEPUKA MIGOGORO NA UKATILI WA KIJINSIA

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajimaleo tarehe 07/05/2022 akizungumza na wafanyabishara wa Soko la Mbezi Luis Dar es salaam ikiwa ni kuelekea Siku ya Familia Duniani.

Mmoja wa wafanyabiashara wa soko la Mbezi Luis Dar es salaam, Mwajuma Debe,akiongea wakati wa ziara ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinaia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima kuelekea Siku ya Familia Duniani.

 ************


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameiasa jamii kupitia familia zao kuweka utamaduni wa kuzungumza masuala mbalimbali yanayowahusu ili kuepukana na migogoro na uwepo wa vitendo vya ukatili katika jamii.


Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo Mei 7, 2022 Mkoani Dar es Salaam kwenye soko la Mbezi Loius akizungumza na wananchi kuelekea maadhimisho ya  Siku ya Familia kwa Mwaka 2022.


Dkt. Gwajima aliongeza kuwa Siku ya Familia Duniani itakuwa na maana zaidi kama jamii yenyewe ikiwa itazungumza kwani inakadiriwa kuwa, ukatili kwa watoto umekuwa ukiripotiwa kufanyika zaidi nyumbani kwa asilimia 60 na shuleni kwa asilimia 40 kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Ukatili dhidi ya Watoto ya mwaka 2011 iliyofanywa na Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la UNICEF.


Waziri Dkt. Gwajima alisema Siku hiyo inaadhimishwa tarehe 15 Mei, na kwa mwaka huu kila Mkoa itaadhimisha Siku hiyo kwenye maeneo yao kwa kuzingatia maelekezo kutoka Wizara kwa  kuitisha makongamano ya kujadili namna ya kuisadia jamii katika malezi katika familia ili kuwa na familia bora na zenye ustawi.


Aidha Dkt. Gwajima alisema kwa upande wa Wizara itaungana na Mkoa wa Dodoma, yalipo Makao Makuu ya nchi na Mgeni Rasmi atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.


Akizungumza kwenye ziara hiyo Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto, Sebastian Kitiku alisema, wameamua kumleta Mhe. Waziri kwenye Soko kwani wanaimani kabisa ni sehemu ambapo makundi yote kutoka kwenye Familia yatafikiwa.


”Kwa kuwa maadhimisho ya mwaka huu ni siku ya Jumapili ambayo siyo siku ya kazi, ni Imani yangu wazazi watatumia siku hii kwenda ibada na familia zao na wale ambao siku hiyo siyo ya ibada kwao, watakaa karibu na familia zao na kutafakari na kuzungumza pamoja juu ya maendeleo na ustawi wa familia zao huku wakifuatilia vipindi mbalimbali vya maadhimisho” alisema Dkt. Gwajima.


Naye Mwajuma Debe Mfanyabisahara soko la Mbezi Luis alisema kulegalega kwa malezi ya Familia, kumetokana na jamii kubadili mtindo wa Maisha ikiwepo Mtoto kulelewa na Familia pekee badala jukumu hilo kuwa la jamii nzima.


“Sisi wakati tunakuwa, ilikuwa huwezi kumpita mtu mzima bila kumsalimia au kumpokea mzigo aliobeba au kumpisha kwenye vyombo vya usafiri, haya ni malezi ambayo yamepotea ndani ya jamii, mtoto miaka ya nyuma alikuwa mtoto wa jamii kinyume na sasa, ukimuadhibu mtoto wa mwingine mzazi wake anaweza kukushambulia kwa maneno makali sana kwa sasa” alisema Mwajuma


Pia Mfanyabishara na Mtaalam wa Elimu Maalum usonji na Upofu, Samwel Mohonge, alisema kinachokuoseka kwa sasa ni elimu jumuishi ya malezi, ambapo alisema jukumu kubwa la malezi jumuishi nikuona kila mwana jamii anakuwa mstari wa mbele kuonya na kukemea.


Kwa upande wake Mfanyabishara kwenye Soko hilo la Mbezi Luis Mwajabu Hassan, alisema kwa sasa suala la kamari limeteka watoto walio wengi kutokana na wazazi kukosa muda wakukaa na familia zao na kujua maendeleo yao.


“Kuna hili suala la (Play Stations-PS), watoto wanakwenda kwenye majumba ya Sinema na Mzazi ukiletewa taarifa wewe hujali na kama wewe ni mkali basi hata hizo taarifa huwezi kupata, hivyo nawaomba wazazi wenzangu na Serikali yetu, tuifanye jumamosi iwe siku ya Familia, sio kusubiria Sikukuu peke yake” alisema Bibi Mwajabu.


Siku ya Familia kwa Mwaka 2022 inaongozwa na kaulimbiu “Dumisha Amani na Upendo kwa Familia Imara; Tujitokeze Kuhesabiwa.” Kauli mbiu hii inaleta Dhahiri Amani na Upendo katika Familia vinavyowezesha familia kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya watoto kiafya, kielimu kimaadili na katika shughuli za kiuchumi. Familia yenye uchumi imara itaweza kumudu kutoa huduma bora za lishe, elimu na ulinzi dhidi ya vitendo vya ukatili.


 MWISHO

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages