Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masalla (wa pili Kulia) akiwa juu ya Tank la maji wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa maji uliopo Kata ya Kiseke Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela leo Jumatatu Mei 09, 2022.
Muonekano wa Tank la maji ambao ni mradi wa maji uliopo katika kata ya Kiseke Mkoani Mwanza.Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masalla akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Kabambo leo Jumatatu Mei 09, 2022 alipofanya ziara yake katika Kata ya Kiseke Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masalla akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Kabambo leo Jumatatu Mei 09, 2022 alipofanya ziara yake katika Kata ya Kiseke Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Kabambo leo Jumatatu Mei 09, 2022 wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela katika Kata ya Kiseke Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.
Wananchi wa Mtaa wa Kabambo wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masalla leo Jumatatu Mei 09, 2022 wakati wa ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela katika Kata ya Kiseke Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.
Picha na Samir Salum
***************
Na Samir Salum, Lango la Habari
Masalla ametembelea mradi huo leo Jumatatu Mei 09, 2022 ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi katika Kata Zilizopo wilayani ilemela Mkoani Mwanza.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo Dc Masalla amesema kuwa lengo la serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha inamtua mama ndoo kichwani kwa kutatua kero za maji na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa kutoa shilingi Milioni 365 ili kutekeleza mradi huo.
“Mwaka jana nlifanya ziara katika kata hii na kero kubwa kutoka kwa wananchi ilikuwa ni ukosefu wa maji, namshukuru Mheshimiwa Rais samia kwa kutoa shilingi 365, pia nimshukuru Mbunge wetu Dkt Angeline Mabula kwa kufikisha kero hii” amesema Dc Masalla
Amesema kuwa Julai 17, 2022 Mwenge wa Uhuru utatembelea mradi huo hivyo amewataka Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati ili kufikia Mei 30, 2022 wananchi waanze kupata huduma ya maji.
Kwa upande wake Mhandisi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) Yustas Karokora amesema kuwa mradi huo unagharimu Shilingi Milioni 365 huku hadi sasa ukiwa umefikia asilimia 88 ukitarajiwa kukamilika mwishoni Mwa mwezi May 2022 na utahudumia wananchi zaidi ya 3500 wa Kata ya Kiseke.
Aidha Mkuu huyo wa wilaya amefanya mkutano wa hadhara katika kata ya kiseke kwa lengo la kusikiliza changamoto mbalimbali za wananchi wa kata hiyo ambapo wamelalamikia kutosomewa taarifa ya mapato na matumizi ya mradi wa maji ya matenki ya plastiki yaliyopo katika mtaa wa kabambo hali inayowapa mashaka.
Akizungumzia kero hiyo mmoja ya wananchi Mtaa wa Kabambo, Lukombwe Ngariba amesema kuwa tangia mradi wa wa maji ya matenki ya plastiki uanzishwe hawajawahi kusomewa taarifa ya mapato na matumizi hali iliyopelekea kutoelewana baina ya wananchi na viongozi.
“tangia huu mradi uwepo hatujawahi kusomewa taarifa ya mapato na matumizi hata siku moja, kila tukikaa vikao tunapigwa tarehe mara kamati iliyoteuliwa inasema haijajiandaa sasa tunabaki kulaumiana na viongozi” amesema Ngariba
Kutokana na changamoto hiyo DC Massala amewataka Viongozi wa Kata ya Kiseke na Kamati iliyokabidhiwa mradi huo kupeleka Nakala ya Taarifa ya mapato na matumizi ofisini kwake na kuhakikisha Siku ya Jumatano Mei 11, 2022 wanafanya mkutano wa hadhara na kuwasomea wananchi taarifa hiyo.
Mwisho