Breaking

Sunday, 8 May 2022

DC BASILLA APATA AJALI





MKUU wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, Basilla Mwanukuzi amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga, Bombo baada ya kupata ajali ya gari.

Akithibitisha Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, David Mwasimbo amesema ajali imetokea usiku wa kuamkia leo Mei 08, 2022 eneo la Hale lililopo Korogwe katika Barabara ya Tanga-Segera.

"Mkuu wa Wilaya anaendelea vizuri isipokuwa dereva wake hali si nzuri, chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi, dereva alikuwa anajaribu kuyapita magari mengine na ndipo ajali ikatokea,"amesema Kaimu Kamanda huyo.

Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Bombo, Dkt. Jonathan Gudemo amekiri kuwapokea majeruhi watatu wa ajali hiyo akiwemo mkuu huyo wa wilaya.

Dkt.Gudemo amesema, majeruhi wawili hali zao zinaendelea kuimarika akiwemo Mkuu wa Wilaya na bado wapo chini ya uangalizi wa matabibu.

"Majeruhi mmoja tumempatia rufaa ya kwenda Muhimbili (Hospitali ya Taifa Muhimbili) kwa ajili ya matibabu zaidi" amesema Dkt.Gudemo.

Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani mara kwa mara wamekuwa wakisisitiza kuhusu umuhimu wa kuzingatia kanuni, tararibu na sheria za usalama barabarani.

Pia wamekuwa wakiwataka madereva bila kujali wanaoendesha viongozi kuepuka mwendokasi kwa kuwa ni moja ya chanzo cha ajali za mara kwa mara.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages