Breaking

Saturday, 7 May 2022

BREAKING: WAZIRI MKUU AZUIA PASSPORT ZA RAIA SABA WA KOREA WAHANDISI WA MV MWANZA "HAPA KAZI TU"




Waziri mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza idara ya uhamiaji mkoani Mwanza kuzuia kwa muda hati za kusafiria za raia saba wa Korea wanaojenga meli ya MV Mwanza “Hapa kazi tu” ili wasiondoke nchini hadi wakamilishe ujenzi wa meli hiyo.

Majaliwa amechukua uamuzi huo leo Jumamosi Mei 7, 2022 Mkoani Mwanza wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa meli hiyo na kugundua ukiukwaji wa makubaliano ya mkataba wa ujenzi wa meli hiyo.


Miongoni mwa maeneo ambayo waziri mkuu amebaini ukiukwaji wa mkataba ni pamoja na kampuni ya Korea ya Gas Entec iliyo na jukumu la kujenga meli hiyo kuuza sehemu ya jukumu la ujenzi kwa kampuni nyingine sababu iliyochangia ujenzi wa meli hiyo kufikia asilimia 65 pekee badala ya asilimia 95 iliyotarajiwa kwa mujibu wa makubaliano ya muda uliotolewa wa kukamilisha kazi hiyo.


Mbali ya hilo, kampuni hiyo pia inadaiwa kupunguza wafanyakazi kutoka 118 hadi kufikia 22 hali inayosababisha ujenzi huo kusuasua licha ya serikali kulipa fedha za ujenzi huo kwa asilimia 80.



Ujenzi wa meli hiyo unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 97.5.


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa yupo Mkoani Mwanza kwa ziara ya kikazi ya siku moja ambapo pamoja na mambo mengine atakagua ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi.

Aidha atakagua Ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema pamoja na kuzungumza na watumishi na wananchi wa Halmashauri hiyo.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages