Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa ametoa siku saba kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Amos Makalla kukutana na LATRA, Wadau na Wamiliki wa Mabasi kuweka uratibu mzuri wa kusimamia maelekezo ya Serikali kwa Mabasi yote kushusha na kupakia abiria ndani ya Kituo kikuu cha Mabasi cha Magufuli - Dar es salaam.
Bashungwa ametoa maelekezo hayo leo mei 30, 2022 wakati akikagua mradi wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli “Magufuli Bus Terminal” kilichopo wilaya ya Ubungo Dar es salaam, amesema Serikali imetumia kiasi cha shilingi bilioni 50 kujenga kituo hicho hivyo Serikali haitakubaliana na watu ambao hawazingatii utaratibu uliowekwa katika kituo hicho.
“Ninafahamu kuwa Mkuu wa Mkoa, Amos Makalla ameshapokea changamoto ya Mabasi kutoingia ndani ya kituo hiki cha Mgugufuli na mimi nimekuta changamoto bado iko pale pale, sasa kwa sababu ameshanza kulifanyia kazi nampa siku saba awe amekutana na LATRA pamoja na wadu wa mabasi (TABOA) kuangalia utaratibu wa mabasi yote kuingia nani ya kituo kushusha na kupakia abiria” amesema Bashungwa.
Halkadhalika Mhe. Bashungwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya Ubungo, Kheri James kuweka utaratibu wa kukutana mara kwa mara na Wadau wa Kituo cha Magufuli, Mawakala na Makalani ili kusikiza na kuweka utaratibu wa kutatua changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza katika kituo hicho na kuzifanyia kazi kwa ushirikiano.