Breaking

Thursday, 26 May 2022

BASHUNGWA ATOA ONYO KALI KWA WATUMISHI WA AFYA WENYE LUGHA CHAFU KWA WAGONJWA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa amewaagiza Waganga Wakuu Wa Mikoa kusimima nidhamu ya watumishi katika vituo vya kutolea huduma za afya msingi ikiwemo kutumia lugha mbaya na isiyo rafiki kwa wagonjwa wakati wa utoaji huduma.


Bashungwa ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma katika kikao cha kujadili utekelezaji wa Mkataba wa afua za lishe nchini  kilichowashirikisha  Waganga wakuu wa Mikoa, Maafisa lishe wa Mkoa  na wadau wa lishe, leo Mei 26, 2022.


Waziri Bashungwa amesema alipokuwa mkoa Mara alikutana na kero za wananchi wakilalamikia baadhi ya wahudumu wa afya kutumia lugha chafu kwa wagonjwa.


“Kwenye ziara zangu nimekuwa nikikumbana na kero za wananchi wakati wakipatiwa huduma ikiwemo kauli zisizo rafiki kwa baadhi ya Wauguzi kwa wagonjwa na nitumie nafasi hii kuwaelekeza Waganga Wakuu wa Mikoa kuendelea kusimamia nidhamu ya watumishi katika vituo vyetu vya kutolea huduma” amesema Bashungwa


Bashugwa ameeleza kumekuwepo na changamoto ya kutopatikana kwa baadhi ya madawa ya kutosha ambapo Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya wanaendelea kufuatilia na kuhakikisha fedha zilizopelekwa Wizara ya afya kupitia MSD yanapatikana madawa ya kutosha katika vituo vyote vya huduma za afya.


Aidha, Amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa kuendelea kusimamia sehemu yao na kukwamua utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayosuasua katika sekta ya afya ikiwemo ujenzi zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya na kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa Watanzania.


Vile vile, Bashungwa amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kutenga fedha kiasi cha shilingi 1000 kwa kila mtoto aliye chini ya umri wa  miaka mitano kwa ajili ya afua za lishe, pia kuhakikisha Mkataba wa lishe unatekelezwa kikamilifu na unakuwa dhana ya kutatua changamoto na kuleta tija kwa Watanzania.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages