Breaking

Wednesday, 4 May 2022

AMUUA MKEWE KISA KAZIDISHA CHUMVI KWENYE CHAKULA




Polisi nchini India wamemkamata mwanaume mwenye umri wa miaka 46 ambaye anadaiwa kumuua mkewe kwa sababu kifungua kinywa chake kilikuwa na chumvi nyingi.

''Nikesh Ghag, karani wa benki huko Thane, karibu na mji wa magharibi wa Mumbai, alimnyonga mke wake mwenye umri wa miaka 40 kwa hasira kwa sababu chakula kinachofahamika kama khichdi ya sabudana [tapioca lulu au sago] alichokuwa anamuandalia kilikuwa na chumvi nyingi,'' afisa wa polisi Milind Desai, aliambia BBC.

Mtoto wa wanandoa hao mwenye umri wa miaka 12, ambaye alishuhudia uhalifu huo, aliwaambia polisi kwamba baba yake alimfuata mama yake, Nirmala, chumbani akilalamikia chumvi iliyopitiliza kwenye chakula na kuanza kumpiga.

''Aliendelea kulia na kumwomba babake awache anachofanya,'' Bw Desai alisema, ''lakini mshtakiwa aliendelea kumpiga mkewe na kumnyonga kwa kamba''.

Baada ya Bw Ghag kutoka nje ya nyumba kwa nguvu, mtoto huyo aliwaita bibi yake mzaa mama na mjomba wake.

''Kufika eneo la tukio, familia yake ilikuwa imemkimbiza hospitalini, lakini wakati huo alikuwa tayari amefariki,'' Bw Desai alisema.

Baadaye mshtakiwa alijisalimisha katika kituo cha polisi, ambapo aliwaambia maafisa kuwa anasumbuliwa na shinikizo la damu.

Alipelekwa jela.

Familia ya Nirmala iliambia polisi kwamba Bw Ghag amekuwa akizozana naye kuhusu ''maswala ya nyumbani'' kwa siku 15 zilizopita.

Bw Desai alisema hawajapokea malalamishi yoyote kuhusu hili kutoka kwa mwathiriwa au familia yake.

Mauaji ya mwanamke na mumewe, yaliyochochewa na ugomvi juu ya chakula, mara kwa mara yanagonga vichwa vya habari nchini India.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages