Jeshi la Polisi mkoani Kagera nchini Tanzania linamshikilia Michael Martini (30) mkazi wa kata ya Nshambya Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera kwa tuhuma ya kuwabaka watoto watatu wenye umri kati ya miaka 10 na 12 wa darasa la tau na la nne wa shule ya msingi iliyopo Bukoba.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani humo, Maketi Msangi akizungumza na waandishi wa habari Mei 26, 2022 amedhibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa ukatili huo ulifanyika Februari mwaka huu wakati watoto hao walipokuwa wameenda kuchanja kuni katika msitu wa Serikali wa Rwendimi uliopo kata ya Ijuganyondo Manispaa ya Bukoba.
Msangi amesema siku ya tukio mtuhumiwa aliwavizia akawakamata na kuwatishia kuwakata kwa panga kama watapiga kelele na kisha kuwabaka.
“Mara baada ya kufanya kitendo hicho cha kikatili mtuhumiwa alikimbia kusikojulikana kuogopa kukamatwa hata hivyo watoto hao walimtambua kwa sura mtuhumiwa huyo,” amesema Msangi.
Amesema jeshi hilo liliendelea na juhudi za kumsaka na Mei 24, 2022 walimkamata mtuhumiwa majira ya jioni katika Kijiji cha Kyansozi kata ya Maruku Bukoba vijijini.
Amesema baada ya upelelezi kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.
Wakati huo huo, jeshi hilo linawashikilia watu wanne ambao ni Hussein Abdallah (46), Mohamed Seleman (24), Richard Juma (20) wote wakazi wa Bukoba na Japheth Pastory (19) mkazi wa Geita kwa tuhuma za kupatikana na injini tatu za boti zenye thamani ya a Sh15.5 milioni.
Baada ya polisi kuwahoji watuhumiwa hao wameeleza kuwa walikuwa wanawateka wavuvi ziwa Victoria kisha kuwatishia na kuwanyanganya boti hizo.