Watu 27 wamefariki dunia na wengine 12 kujeruhiwa baada ya moto kutokea katika jengo lenye ghorofa nne Jijini Delhi Nchini India, Polisi wamesema kulikuwa na watu zaidi ya 70 katika jengo hilo.
Moto huo mkubwa ulizuka jana Ijumaa Mei 13, 2022 majira ya Alasiri, huku chanzo kikidaiwa kuwa ni shoti ya umeme kwa kuwa jengo halikuwa na miundombinu mizuri ya umeme
Picha za televisheni zilionyesha moshi ukifuka kutoka kwenye madirisha ya jengo hilo, huku wazima moto wakiwasaidia wale waliokwama kwenye orofa za juu kutoroka huku mamia wakitazama. Zaidi ya magari 30 ya zimamoto yalikuwa kwenye eneo la tukio, pamoja na gari la Wagonjwa.
"Miili 27 iliyoungua ilipatikana kutoka kwa jengo hilo na karibu dazeni mbili za majeruhi wanaendelea na matibabu," alisema Satpal Bharadwaj, ambaye alikuwa msimamizi wa shughuli za zima moto huko Delhi katika eneo la tukio.
Moto huo ulizuka katika ghorofa ya kwanza ya jengo ambalo ni ofisi ya kampuni ya utengenezaji wa kamera za uchunguzi, polisi walisema.
Jeshi la Polisi Delhi Limeeleza kuwa leo Jumamosi Mei 14, 2022 wamewakamata wamiliki wawili wa kampuni hiyo na kueleza kuwa wanakabiliwa na kesi ya mauaji bila kukusudia na njama za uhalifu ambayo inaweza kuadhibiwa kwa kifungo cha maisha au miaka 10 jela.
Mkurugenzi wa huduma ya zima moto ya Delhi Atul Garg amesema kuwa Jengo hilo halikuwa na kibali kutoka kwa idara ya zima moto na halikuwa na vifaa vya usalama wa moto kama vile vizima moto.
Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi ametoa pole na kuahidi kutoa Dola 2,580 (Tsh milioni 5.9) kwa kila familia iliyopoteza ndugu katika tukio hilo