Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amewataka wachezaji wa timu ya Taifa ya Wanawake chini ya miaka 17 - Serengeti Girls kucheza kwa juhudi kama wanacheza fainali kwa kila mchezo wa hatua ya kufuzu kombe la Dunia.
Waziri Mchengerwa ameyasema hayo leo Alhamisi April 14, 2022 wakati akizungumza na wachezaji na benchi la ufundi kwa njia ya simu wakati timu hiyo ikabidhiwa bendera ya Taifa na Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul kwenye mpaka wa Burundi na Tanzania muda mfupi kabla ya kuelekea nchini Burundi kwa ajili ya mchezo wa kuwania kufuzu kombe la dunia dhidi ya timu ya Taifa ya Burundi.
"Hakikisheni mnakwenda kucheza kwa ari, ujuzi na maarifa na kila mchezo muupe umuhimu kama mnacheza fainali ili mtuletee heshima, Watanzania wanamatumaini na imani kubwa kwenu" amefafanua, Mhe. Mchengerwa

"Serikali ipo nanyi bega kwa bega na inafuatilia kwa karibu ushiriki wenu, kufuzu kwenu kwa mara ya kwanza kushiriki mashindano haya itakuwa chachu kwa timu nyingine za Taifa kuiga mfano wenu na kuendelea kupeperusha vizuri bendera ya nchi yetu" - Mchengerwa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul ambaye anaongoza msafara wa timu hiyo nchini Burundi amewatia moyo wachezaji pamoja na benchi la ufundi kuwa amesafiriki umbali wa zaidi ya kilomita elfu moja kwa barabara kutoka Dodoma hadi Ngozi nchini Burundi kuhakikisha kuwa wanashinda mchezo huu muhimu.

Timu hiyo inatarajia kucheza mchezo wa kuwania kufuzu kombe la Dunia jumamosi tarehe 16 Aprili, 2022 saa kumi jioni kwa saa za Tanzania.