Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa ameitaka Bodi ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) aliyoiteua hivi karibuni, kuifanya michezo nchini kuwa biashara badala ya kuendelea na mazoea ili kutoa ajira na kuchangia kwenye uchumi wa nchi.
Waziri Mchengerwa ameyasema haya leo Jumatano Aprili 20, 2022 kwenye Ukumbi wa Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam wakati aikizindua rasmi Bodi hiyo ya 15 ya BMT ambapo amefafanua kuwa kazi kubwa ya Bodi hiyo ni kuisaidia Serikali kuandaa timu bora za taifa katika michezo mbalimbali ili ziendelee kufanya vizuri katika michezo kimataifa.
Ameitakia Bodi hiyo kuwa na mikakati kabambe ya kuwashirikisha wawekezaji kutoka sehemu mbalimbali kuja kuwekeza kwenye miundombinu ya michezo ili kuhakikisha kuwa michezo inapiga hatua.
Ameiagiza Bodi mambo matatu ili kuendeleza michezo nchini huku akisisitiza kuwa mwamko uliopo leo kwenye michezo ni maono na Jitihada zilizoanza tangu tarehe 9 Disemba, 1961 Taifa la Tanzania lilipopata uhuru chini ya Uongozi Shupavu wa Hayati Mwl. J.K. Nyerere
“Jambo la kwanza nendeni mkaimarishe na kusimamia fedha za mfuko wa maendeleo ya michezo kwa kuhakikisha kuwa malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa. Malengo hayo ni pamoja na kuhakikisha timu za Taifa zinahudumiwa na kuratibiwa ipasavyo, miundombinu ya michezo inaboreshwa na kujengwa, wataalamu wa michezo wanapewa mafunzo yanayostahili ili kuendana na hali halisi halisi Duniani, lakini pia kuanzisha program zitakazoibua vipaji kwa vijana wetu, ili tuwe na timu za Taifa zenye ushindani na kutoa fursa za ajira kwa vijana wetu”. Amefafanua Mhe. Mchengerwa
Waziri Mchengerwa ameeleza Jambo la pili kuwa kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato vitakavyotunisha mfuko wa maendeleo ya michezo ili kukidhi mahitaji ya michezo ambapo suala la tatu amelitaka Baraza kuhakikisha linakuwa na mkakati madhubuti wa kuimarisha utawala bora na utendaji kazi wenye weledi kwa viongozi wa vyama, mashirikisho, kamati na vilabu vya michezo nchini.
Aidha suala tatu ni utawala bora ambapo waziri Mchengerwa ameeleza kuwa ndio jambo la kuanza nalo na ameitaka Bodi kuyaita mashirikisho yote ya michezo ili kuyaelimisha kuepuka vitendo vyovyote vya rushwa na upendeleo na kuhakikisha wanazingatia na kufuata, miongozo na taratibu za nchi, sambamba na kuziheshimu mamlaka na Taasisi zinazosimamia michezo.
Akitoa neno la shukrani kwa Mhe. Waziri Mchengerwa, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Leodgar Tenga amesema kuwa bodi yake ipo tayari kufanya kazi na itatumia hotuba yake kama mwongozo wa kwanza wa kufanyia kazi.