Waziri wa Maji Jumaa Aweso amefanya kikao na Wadau wa Sekta ya Maji wa Handeni na kuelekeza hatua za haraka kuchukuliwa ikiwemo kusimamishwa kazi kwa Watumishi wanne wa Wizara ya Maji kutokana na kusuasua kwa kazi ya ujenzi wa bwawa la Kwankambala.
Kikao hicho kilichofanyika Dodoma na kuhudhuriwa na Viongozi wa Wilaya ya Handeni ni moja ya hatua zilizochukuliwa baada ya ziara ya kikazi ya Aweso Wilayani hapo 12 April, 2022 ambapo ilibainika kwamba Injinia anayejenga bwawa hilo amelipwa Shilingi milioni 602,859,075.66 sawa na 33% ya gharama ya mkataba na kazi iliyofanyika ni asilimia 20 tu.
Vilevile iligundulika kwamba kampuni iliyopewa kandarasi ya kazi hiyo iitwayo Civil Loth Enterprises Ltd iliondoa vifaa vya kazi katika eneo la ujenzi, ingawa ilikuwa imeongezewa muda wa utekelezaji wa ujenzi na kutokana na hali hiyo, kikao kilichoongozwa na Aweso kimeelekeza yafuatayo kufanyika kwa mapitio ya Mkataba wa nyongeza wa Mkandarasi.
Pia amewasimamisha kazi Watumishi wanne ili kupisha uchunguzi.
Watumishi hao ni Msimamizi wa Mradi – RUWASA Makao Makuu Hamisi Matungulu, na Mhasibu Mkuu – RUWASA Makao Makuu Jimmy Mwanyakunga.
Wengine ni Amos Mtweve ambaye ni Meneja Udhibiti Ubora wa Miradi na Mwenyekiti wa Bodi ya Manunuzi RUWASA Makao Makuu), Zam Mlimira (Mkurugenzi wa Manunuzi na Ugavi – RUWASA Makao Makuu).