Watu wawili wamefariki dunia katika ajali iliyohusisha Basi la Kampuni ya Buti la Zungu kugonga pikipiki katika eneo la Nangurukulu Wilayani Kilwa Mkoani Lindi.
Akithibitisha tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi RPC Mtatiro Kitinkwi amesema ajali hiyo imetokea leo Jumatano April 20, 2022 ikihusisha basi la kampuni ya Butila zungu lenye namba T.501 BRU kugongana na pipikipiki namba MC.109 CPX iliyokuwa na kusababisha vifo vya dereva wa pikipiki hiyo na abiria wake.
"Pikipiki ilikuwa ikiendeshwa na Jafari Madega (30) akiwa amembeba abiria aitwaye Athuman Madega (58) ambaye ni Mfanyakazi wa TANESCO Wilayani Kilwa, Dereva huyu wa pikipiki na abiria wake ndio ambao wamefariki kwenye ajali hiyo, wote wamefia palepale kwenye eneo la tukio" amesema RPC Mtatiro
Kamanda ameeleza kuwa uchunguzi umeonesha dereva wa pikipiki alihama upande wake na kwenda upande wa basi hilo na kupelekea kutokea kwa ajali hiyo na kuongeza kuwa miili ya Marehemu imehifadhiwa Kituo cha Afya Kilwa Masoko.
Dereva wa basi hilo anaendelea kushikiliwa na jeshi la polisi kwa uchunguzi zaidi.