Shirika la umeme nchini Kenya linasema linapoteza mamilioni ya dola kwa mwezi kutokana na uharibifu wa transfoma zake za umeme unaotokana na wizi wa mafuta yake ambayo nayauzwa kama mafuta ya kupikia nchini humo.
Kampuni ya Kenya Power imesema kuwa wahalifu huchota mafuta hayo kutoka kwenye transfoma, na kuuzwa kwenye migahawa na vibanda vilivyo kando ya barabara kwa ajili ya kukaanga vyakula.
Wizi huo umeongezeka siku za hivi karibuni ambapo umehusishwa na kupanda kwa gharama ya mafuta ya kupikia.
Wataalamu wa afya wanaonya kuwa mafuta ya transfoma ambayo yanaonekana kama mafuta ya kupikia si salama kwa matumizi ya binadamu na yana hatari kubwa kiafya.
Taarifa iliyotolewa na Kenya Power ilibainisha kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la uharibifu katikati mwa Kenya, ambapo karibu transfoma 20 ziliharibiwa au kuingiliwa.
Harrison Kamau, meneja wa biashara wa kampuni hiyo katika Kaunti ya Murang’a, alieleza kuwa mtuhumiwa mmoja “alinaswa na umeme akiwa juu ya transfoma alipokuwa akijaribu kuondoa/kurudisha fusi Kwa sasa amelazwa katika Hospitali Kuu ya Thika akiwa na majeraha ya kutishia maisha,"
Kampuni ya Kenya Power sasa imeanza kampeni ya uhamasishaji nchi nzima kuhusu hatari ya kuharibu gridi ya taifa, na hii inajiri huku kampuni hiyo ikikabiliwa na kukatika kwa umeme mara kwa mara.