Breaking

Tuesday, 19 April 2022

WADAU WATAKIWA KUWEKEZA MIUNDOMBINU YA MICHEZO


Na Mwandishi Wetu-Dar es Salaam

 

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa michezo kujitokeza kuwekeza katika miundombinu ili sekta ya michezo iweze kusonga mbele.


Waziri Mchengerwa ametoa wito huo leo Jumanne April 19, 2022  kwenye ufunguzi wa maabara ya kisasa ya Komputa iliyojengwa kwa ufadhili wa klabu ya Baseball Dodgers ya Marekani kupitia Chama cha Mchezo wa Baseball/Softball Tanzania.


Katika tukio hilo lililofanyika kwenye Shule ya Sekondari ya Azania jijini Dar es Salaam Waziri Mchengerwa amemwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ambapo limehudhuriwa na taasisi za michezo wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara  Saidi Yakubu na wadau mbalimbali.



Waziri Mchengerwa amesema kuwa dhamira ya Serikali  ni kuendelea kukuza sekta ya Michezo na Sanaa kwa kushikiana na wadau wenye utashi wa kuwekeza katika sekta hizo.


"Mpango wa Serikali ni kufanya michezo iwe biashara". Amesema Mchengerwa



Amesema tayari Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji na wanamichezo ili kuhakikisha lengo la kuboresha michezo hatimaye kutoa ajira na kuongeza uchumi liweze kufikiwa.


"Nyote mnakumbuka , hivi karibuni Serikali imepitisha Sheria ya uundaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Michezo ambapo kiasi cha asilimia 5 ya fedha zinazitokana na kodi ya michezo zitaingizwa  katika huu ili kuendeleza sekta ya michezo nchini". Amesisita Mhe. Mchengerwa


Ameeleza kuwa  Serikali itaendelea kutatua changamoto ya miundombinu  ya michezo ambapo kwa sasa tayari imetenga  shilingi bilioni 10.5 kwa ajili ya ujenzi wa viwanja vya kupumzikia kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma  na Geita.



Waziri Mchengerwa ameongeza kuwa Wizara yake inakwenda kuratibu kombe la Samia CUP mtaa kwa mtaa na kusisitiza kuwa mashindano hayo  yana lengo la kusaka vipaji vya wachezaji kuanzia ngazi ya chini ya mtaa na kijiji.


Katika hatua nyingine Waziri Mchengerwa amesema Serikali ya Rais Samia  kupitia Wizara yake imechangua Shule ya Azania na Kibasila katika mkoa wa Dar es Samaam ili zijengewe  miundombinu ya michezo katika program ya kujenga shule mbili za michezo kila mkoa.


"Hivi ninavyosema tayari tumetengewa bilioni mbili kwa ajili ya kazi hiyo na ninaagiza hapa  Azania iwe shule ya kwanza kujengewa miundombinu hiyo" amesisitiza Mhe. Mchengerwa



 Aidha, Waziri Mchengerwa amepata fursa kuangalia timu ya taifa ya baseball ikifanya mazoezi katika uwanja wa shule ya Azania


Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages