WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema masuala ya ufuatiliaji na tathmini yanapaswa kupewa kipaumbele ili Taifa liendelee kupata matokeo yanayokusudiwa katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo.
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo leo Jumatano, Aprili 27, 2022 wakati akifungua Kongamano la Kwanza la Kitaifa la Wiki ya Ufuatiliaji na Tathmini lililofanyika katika ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amesema kuwa kongamano hilo linaakisi maono na maelekezo ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu kuimarisha tasnia ya ufuatiliaji na tathmini.
Waziri Mkuu amesema tayari Serikali imeandaa mwongozo wa ufuatiliaji na tathmini ya miradi na programu za maendeleo unaoainisha majukumu na wajibu wa kila mdau katika usimamizi wa miradi.
Amesema mwongozo huo ambao umesambazwa katika Wizara, Halmashauri na taasisi zote za Serikali utaanza kutumika katika mwaka wa fedha 2022/2023. Mwongozo wa Taifa wa Ufuatiliaji na Tathmini ya miradi umeainisha umuhimu wa kushirikisha wananchi katika hatua zote za utekelezaji wa miradi.
Amesema ni vyema nchi kuwa na mfumo wa ufuatiliaji na tathmini unaotoa fursa ya kushirikisha wananchi na wadau wengine ili kuongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali na sekta binafsi.
“Kwa kufanya hivyo, tutatoa nafasi ya kupima utendaji kwa ujumla na hivyo, kujua tumefikia wapi, tumekwama wapi na wapi tunahitaji kufanya maboresho. Lengo kuu ni kufikia malengo tarajiwa.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa wananchi wakiwa na fursa ya kufuatilia na kuhoji utekelezaji wa yale tunayoyaahidi hakika uwajibikaji utaongezeka.
Amesema Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22-2025/26) unachangia kufikia Ajenda ya Maendeleo ya Afrika ya mwaka 2063, Dira ya Maendeleo ya Afrika Mashariki ya mwaka 2050 na Ajenda ya Dunia ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema bila kuwa na usimamizi madhubuti wa eneo la ufuatiliaji na tathmini itakuwa vigumu kwa nchi yetu kuelewa iko wapi katika utekelezaji wa mipango yote kwa ujumla.
“Kwa kuzingatia kwamba nchi yetu ni sehemu ya Afrika na Dunia, tunaungana na nchi nyingine duniani katika kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ambayo imepewa kipaumbele katika utekelezaji wa mipango ikiwemo niliyoitaja hapo juu.”