Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa kesho, Aprili 2, 2022 anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye hafla ya utoa wa Tuzo za Muziki Tanzania 2021 katika Ukumbi wa Mkutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Matiko Mniko, maandalizi yote ya msingi yameshakamilika kwa ajili ya shughuli hiyo.
Ameeleza kuwa leo wataalam mbalimbali walioratibiwa na BASATA wanakutana na washiriki ili kuwapa semina na utaratibu wa shughuli nzima ya kesho ya utoaji wa Tuzo za Muziki.
Amesema toka zoezi la upigaji kura lililoanza Machi 20 mwaka huu na tayari zaidi ya wapenzi na mashabiki wa muziki zaidi ya 90000 wameshapiga kura ambapo amefafanua kwamba zoezi hilo litakoma leo Aprili 1 majira ya saa sita usiku.
Amesema kesho Aprili 2, 2022 kwenye usiku huo wa utoaji wa tuzo utapambwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali, bendi na vikundi vya ngoma ambapo tuzo 51 zitatolewa.
Mniko amesema Tuzo za muziki Tanzania zilianzishwa mwaka 1999 na Baraza la Sanaa la Taifa likiwa chini ya Wizara ya Sanaa na Utamaduni na zikaacha kutolewa mwaka 2015 kutokana na sababu mbalimbali.
Amesema Serikali imeamua kurudisha tuzo hizi ikiwa na malengo ya kukuza wanamuziki wa Tanzania na kazi zao, kuimarisha ubora katika kazi za muziki, kukuza vipaji vya wanamuziki chipukizi na kuimarisha mahusiano kiutendaji kati ya Baraza wanamuziki na wadau wa wanamuziki katika maendeleo ya Muziki Tanzania.
Amesema mchakato wa kuwapata washindi wa mwaka huu umefanywa na weledi wa hali ya juu kwa kuwatumia wataalam wabobezi katika sekta hiyo ambapo amesema kaulimbiu ya mwaka huu ni “Muziki wetu Tuzo zetu”.
Tukio hili litarushwa mubashara kwenye vyombo mbalimbali vya ndani na nje.