
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema kuwa katika kipindi cha robo tatu kuanzia mwezi July 2021 hadi March 2022 kwa mwaka wa fedha 2021/22 imekusanya Tsh. Trilioni 16.69 ikiwa ni sawa na ufanisi wa 97.3% ya lengo la kukusanya Tsh. Trilioni 17.15.
Katika Taarifa iliyotolewa leo Jumapili April 03,2022 na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata amesema kuwa makusanyo haya ni ongezeko la Tsh. Trilioni 3.1 ukilinganisha na kiwango cha makusanyo cha Tsh. Trilioni 13.59 kilichokusanywa kwa kipindi kama hiki kwa mwaka wa fedha 2020/21.
"Ongezeko hili ni ukuaji wa makusanyo ya kodi wa 22.8%"
Aidha kwa mwezi Machi 2022, TRA imekusanya Tsh. Trilioni 2.06 kati ya lengo la kukusanya Tsh. Trilioni 1.98, makusanyo haya ni sawa na ufanisi wa 103.6% na ukuaji wa 23.17% ikilinganishwa na mwezi Machi 2021 ambapo makusanyo yalikuwa Tsh. Trilioni 1.67
Kidata ameeleza kuwa makusanyo hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuongezeka kwa uhiari wa kulipa kodi, kuimarika kwa mahusiano baina ya TRA na walipakodi kunakochagizwa na utatuzi wa migogoro ya kodi nje ya mahakama pamoja na kushughulikia malalamiko ya walipakodi kwa wakati, pia ufanisi huo umetokana na kuimarika kwa uzalishaji wa viwanda vya ndani na biashara za kimataifa"
"TRA inapenda kutoa pongezi na shukrani za dhati kwa walipakodi wote na wadau mbalimbali kwa kujitoa kwa dhati katika kuendelea kulipa kodi kwa hiari, kipeke tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia kwa miongozo na msaada wake katika kutekeleza wajibu wetu, ulipaji kodi sahihi wa hiari na kwa wakati kumeifanya TRA ivuke lengo mwezi Machi 2022 na kunaiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake kwa wananchi kama vile kugharamia miradi ya maendeleo, kutoa huduma za kijamii, ulinzi na usalama wa nchi"

