Sakata la madai ya wizi wa kura limeibuka bungeni ambapo Mbunge wa Makambako (CCM), Deo Sanga amesema wananchi wamewapa ushindi wa kishindo kutokana na kazi mbalimbali zinazofanywa.
Sanga ameyasema hayo leo Jumanne Aprili 19, 2022 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) 2022/2023.
“Sasa mheshimiwa Spika nasema kwa uchungu mkubwa, mimi nimeshinda kwa kishindo na waheshimiwa wote hapa wameshinda kwa kishindo sio kwa kuiba kura”amesema.
Amesema huyo anayesema hivyo analengo la kuwagombanisha na wananchi na kwamba ndio maana katika jimbo la Nkasi Kaskazini wameshindwa na akashinda mbunge wa Chadema.
Amesema kuieleza jamii kuwa CCM inaiba kura, jambo ambalo si la kweli na kwamba wanashinda kwa kishindo kwa sababu Watanzania wanakubali na mambo yanayofanywa na Serikali inayoongozwa na chama hicho.
Source: Mwananchi