
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Zoezi la Sensa ya watu na makazi litaanza Rasmi Agosti 23, 2022.
Pia amezindua nembo Rasmi ya Sensa ya watu na Makazi.
Uzinduzi huo wa nembo na tarehe ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, umefanyika leo Ijumaa April 08, 2022 Katika Hotel ya Golden Tulip, Zanzibar.
Katika Uzinduzi huo Rais Samia amesema shughuli ya kuhesabu watu itasaidia Serikali kupanga vyema mipango yake ya maendeleo.
"Serikali haiwezi tu kukaa mezani ikapanga mipango ya maendeleo bila kuwa na takwimu sahihi za watu wapi wapo, wanawake wangapi, wanaume wangapi, watu wenye ulemavu ni wangapi, watoto wangapi na wakubwa wangapi, lazima tuwe na hesabu hizo." Amesema Rais Samia
Aidha ameagiza nembo ya Sansa kutumika katika shughuli zote za kiserikali na taasisi binafsi ili kuhamasisha wananchi waweze kutambua umuhimu wa kihesabiwa.
“Kwa taasisi za Serikali nembo hii iwekwe kwenye machapisho, website na mitandao ya kijamii lakini kwa upande wa taasisi binafsi zinaweza kuwekwa hata kwenye vifungashio au risiti na tiketi, kikubwa kila sehemu tuone hiyo nembo,” amesema Rais Samia
Majaliwa amesema mpaka sasa maandalizi ya shughuli hiyo ya sensa yamefikia asilimia 79 na kwamba kazi hiyo inaendelea kuratibiwa kwa ushirikiano mkubwa kati ya Serikali.
Kwa upande wake Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya sensa amesema kuwa hadi kufikia Machi 31, 2022 maandalizi ya sensa yamefikia asilimia 79.
“Kwa kuwa sensa inafanyika kila baada ya miaka 10, zoezi la sasa litatumika kama rejea kwa miaka 10 ijayo, ndiyo maana tumeshirikisha wadau na litafanyika kwa umakini mkubwa.”
Ameongeza kuwa Serikali imesikia kilio cha viongozi wa dini na kuwa zoezi hilo litafanyika siku za kazi ili kukwepa siku za ibada.