Breaking

Saturday, 30 April 2022

PROFESA KIKULA AWATAKA MAAFISA MADINI WAKAZI WA MIKOA KUONGEZA KASI UKUSANYAJI WA MADUHULI


Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa nchini kuongeza kasi ya ukusanyaji wa maduhuli ikiwa ni pamoja na kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kufikia lengo lililowekwa la mwaka 2021/2022 la shilingi bilioni 650 na Sekta ya Madini kuendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa.


Profesa Kikula ametoa rai hiyo kwenye kikao kazi cha manejimenti ya Tume ya Madini kilichofanyika jijini Dodoma chenye lengo la kujadili utendaji wa Tume pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya utekelezaji wa bajeti na ukusanyaji wa maduhuli kwa mwaka wa fedha 2022/2023.


Sambamba na kupongeza baadhi ya ofisi za maafisa madini wakazi wa mikoa kwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli amezitaka ofisi nyingine kuongeza bidii na ubunifu pamoja na kuendelea kuwa wazalendo kwenye usimamizi wa rasilimali za madini.


Katika hatua nyingine, amewataka watendaji wa Tume ya Madini kuendelea kuimarisha ushirikiano na nidhamu kwenye utendaji kazi hivyo kuendelea kujenga taswira chanya ya Tume ya Madini kwenye jamii.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages