Na Ayoub Julius
Norwich City wameshushwa daraja kutoka Ligi kuu Uingereza baada ya vijana wa Dean Smith kushindwa na klabu yake ya zamani ya Aston Villa.
Yote hayo yanajiri baada ya kipigo cha bao 2-0 dhidi ya Aston Villa mchezo uliochezwa leo Jumamosi April 30, 2022.
Magoli ya mchezo huo yamefungwa na Ollie Watkins na Danny Ings, ikiwa ni kipigo cha 23 msimu huu na kinawahukumu katika kifungo cha daraja la pili baada ya Burnley kujinasua wakitokea nyuma na kuwalaza Watford kwa goli 2-1 katika viunga vya Vicarage Road.
Ni mara ya nne katika misimu minane kwa Norwich kushuka daraja, huku pointi zao za sasa zikiwa sawa na zile za msimu wa 2019/20.
Smith alichukua mikoba ya Daniel Farke mnamo Novemba mwaka jana, baada ya Mjerumani huyo kufukuzwa kwenye wadhifa wake baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Brentford,ushindi wa kwanza wa klabu hiyo katika msimu wa Ligi Kuu ya Uingereza.
Ushindi ulifuatia katika mchezo wa kwanza wa Smith, ushindi wa 2-1 dhidi ya Southampton, lakini Norwich hawajaweza kuongeza kasi tangu wakati huo na sasa wanajikuta wakisaka kupanda tena Ligi kuu Uingereza.