Breaking

Friday, 29 April 2022

NAIBU WAZIRI GEKUL AWATAKA WATANZANIA KUTUMIA FURSA ZA ROYAL TOUR





Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Philipo Gekul amewataka watanzania kutumia fursa iliyotengenezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Samia Suluhu Hassan kwenye Filamu ya Royal Tour.


Gekul ameyasema haya leo Alhamisi Aprili 29, 2022 kwenye semina ya wadau wa sekta ya filamu ya Royal Tour iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Dar es Salaam.



Naibu Waziri Gekul amesema kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana na wanatasnia ya filamu katika kuendeleza Sekta ya filamu nchini ikiwa ni pamoja na kutengeneza mazingira rafiki na wezeshi yatakayo wawezesha wanatasnia wa ndani na nje ya nchi kufanya shughuli zao nchini.


Amesema yapo maeneo kadhaa muhimu ambayo Tanzania inaweza kushirikiana na Marekani katika filamu na ikanufaika nayo.



Ameyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na utayarishaji wa filamu kwa kutumia mandhari zinazo patikana katika nchi zote mbili, Usambazaji (Uuzaji) wa filamu za ndani ambapo amefafanua kuwa ipo haja ya kusambaza filamu zinazozalishwa hapa nchini kwa hadhira kubwa zaidi ikizingatiwa kwamba Tanzania inazalisha takriban filamu 1400 kila mwaka ambazo hurekodiwa kwa lugha ya Kiswahili ambayo inazungumzwa na takribani watu milioni 150 duniani.


Maeneo mengine ni kuwa na eneo Changamani la Filamu na kuandaa matamasha na Tuzo za Filamu za Kimataifa kama vile Tamasha la Filamu la Lake International Pan African la Kenya, Tuzo ya OUMAROU Ganda Price ya Bukina Faso, Tuzo za Hollywood na African Prestigious Awards (HAPAWARDS) za Marekani, Tuzo za World Oscar Signature za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Tuzo za African Magic Viewer’s Choice Awards (AMVCA) za Nigeria, na Tuzo za ZIMOKO za Zambia.



Naye, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Abbasi amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kuiandaa na kwamba watanzania wanapaswa kumpongeza kwa ujasiri na kuwa mstari wa mbele kufanikisha filamu hii.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages