Breaking

Tuesday, 19 April 2022

MWANAUME WA MIAKA 58 ABAKA WATOTO WATATU AKIWEMO BINTI YAKE



Na Samir Salum-lango la habari 

Mwanaume mmoja anaejulikana kwa jina la Simon Zakalia (58) anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za ubakaji wa watoto watatu akiwemo binti yake Wilayani Hanang mkoani Manyara.

Akithibitisha tukio hilo mbele ya waandishi wa habari Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara, Limited Mhongole amesema mtuhumiwa huyo alitenda ukatili huo mwaka 2021 na 2022, mbapo tukio la kwanza anatuhumiwa kumbaka mwanafunzi akiwa shambani.

Kaimu Kamanda Mhongole ameeleza tukio la kwanza kuwa mnamo Juni 2021 katika Kijiji cha Masakita, msichana mwenye umri wa miaka 12, mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Masakita aligundulika amebakwa na mtuhumiwa, baada ya kumvizia wakati akitoka shambani.

"Kumbukumbu zinaonyesha alimlaghai kwamba atampa shilingi mia tano ili asitoe taarifa nyumbani kwao"

Katika tukio la pili amesema kuwa mnamo mwezi Machi 2022, mtuhumiwa alimbaka msichana mwenye umri wa miaka 13 anayeishi na bibi yake ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Masakita ambapo alimpeleka shambani na kumfanyia kitendo hicho.


"Binti huyo anaeishi na bibi yake ambaye alikuwa amesafiri na uchunguzi ukionesha kuwa alishawahi kumbaka Mwezi Novemba 2021" Ameongeza Mongole

Pia, Mnamo Machi, 2022 mtuhumiwa alimbaka mtoto wake wa kumzaa mwenye umri wa miaka 12 ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba ambapo alimlazimisha kufanya kitendo hicho shambani huku akimtishia kuwa atamuua akitoa siri kwa bibi yake anayeishi nae.

Kaimu kamanda Mhongole amesema Chanzo cha kugundulika matukio haya ni mtuhumiwa kumfuata binti yake na kumtaka wafanye mapenzi ndani ya nyumba ya bibi yake, binti akamwambia atangulie shambani anamfuta, baada ya mtuhumiwa kuondoka ndipo binti akatoa taarifa kwa jirani.

"Jirani akamfikishia bibi yake, bibi naye akatoa taarifa shuleni, kikafanyika kikao, binti akawataja wahanga wenzake wawili"

Kamanda Mhongole amesema Mtuhumiwa tayari amekamatwa na yupo mahabusu na atafikishwa Mahakamani uchunguzi utakapokamilika.

Aidha, Kamanda Mhongole ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwa makini na watoto wao kwani uchunguzi unaonyesha kuwa kuna wanaoishi na bibi zao wanafanyiwa udhalilishaji akieleza kuwa baadhi ya walezi wao wanakuwa hawana muda wa kuwaangalia.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages