![]() |
Muonekano wa Tanki la Maji Amani Makoro wilayani Mbinga |
UTEKELEZAJI wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19, kupitia sekta ya maji vijijini mkoani Ruvuma imefikia asilimia 52, hali ambayo inatarajiwa kumtua mama ndoo kichwani.
Mkoa wa Ruvuma unatekeleza miradi saba ya maji ambayo inagharimu zaidi ya Sh.bilioni 4.8 zinazotokana na mkopo usio na riba wa Sh. trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Miradi hiyo katika Mkoa wa Ruvuma inatekelezwa katika majimbo ya Nyasa, Mbinga Mjini, Mbinga Vijijini, Songea DC, Madaba, Namtumbo, Tunduru Kusini na Kaskazini.
Akizungumza na waandishi wa habari ambao wametembelea miradi ya maji inayotokana na fedha za Uviko-19 katika Wilaya ya Nyasa, Mbinga na Tunduru, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingiria Vijiji mkoani Ruvuma (Ruwasa), Mhandisi Rebman Ganshonga amesema miradi hiyo imekuwa kumuondolea mama adha ya kufuata maji mbali.
Ganshonga amesema Ruwasa mkoa wa Ruvuma wamejipanga kuhakikisha miradi yote ambayo inatokana na fedha za Uviko-19 inakamilika kwa wakati na kwamba hawatavumilia mkandarasi ambaye atazembea.
“Sisi Ruwasa Ruvuma tumejipanga kufanikisha lengo la Serikali kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 maji vijijini yanapatikana kwa asailimia 85 na fedha hizi za Uviko-19 zimeweza kuchochea lengo hilo kufikiwa,” amesema.
Meneja huyo amesema pamoja na miradi ya fedha za Uviko-19, pia wanaendelea kutekeleza miradi mingine ambayo imewezesha upatikanaji wa maji vijijini kufikia asilimia 68 kutoka 56 ya awali, huku matarajio yao ni miradi hiyo ikikamilika vijijini maji yatakuwa yakipatikana kwa asilimia 75.
Mhandisi Ganshonga amesema malengo yao ni kuhakikisha miradi hiyo ikikamilika upatikanaji wa maji mijini utafikia asilimia 88, hivyo lengo la kufikia asilimia 95 ya maji mijini ifikapo 2025 itatimia.
Ganshonga amesema wanatarajia maeneo ya mijini kama wilayani Mbinga maji yatakuwa yanapatikana kwa asilimia 100 ifikapo 2025, pamoja na kuwepo na uharibifu wa vyanzo vya maji.
Mhandisi huyo amesema utekelezaji wa miradi unaendelea mkoani hapo unaendana na utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji.
“Ruwasa Ruvuma ni moto wa kuotea mbali, inaupiga mwingi, nadhani mmezunguka huko vijijini mmeona kazi inayoendelea, sisi tutatekeleza miradi kila fedha zinapokuja ili tumtue mama ndoo kichwani.Lakini pia kauli mbiu yetu ya maji bombani lazima itimie. Hatutarajii kumuangusha Rais Samia na Waziri wa Maji Jumaa Aweso,” amesema.
Mwisho