Na Seveline Mbullu-Lango la habari,Kishapu
Mahakama ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela Gangira Makila (37) ambaye ni mganga wa Kienyeji mkazi wa kijiji cha Mpyagula kilichopo Wilaya ya Igunga mkoani Tabora kwa kosa la kubaka mtoto mwenye umri wa miaka 12.
Makila amehukumiwa kifungo hicho leo Alhamisi April 28,2022 baada ya mahakama kumtia hatiani mshtakiwa baada ya kusililiza mashahidi watano akiwemo shahidi namba moja ambaye ni Babu wa mtoto , shahidi wa pili ambaye ni daktari wa hospitali ya Wilaya ya Kishapu huku shahidi mwingine akitajwa kuwa ni jirani wa mtoto pamoja na askari polisi.
Katika shauri namba 170 la mwaka 2021 lililowasilishwa na mwendesha mashtaka wa serikali, Peter Masatu Masau mbele ya Hakimu mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Kishapu, Johanitha Rwehabula anadaiwa kufanya kosa la ubakaji katika halmashauri ya Wilaya ya Kishapu kinyume na kifungu cha sheria namba 130 kifungu kidogo cha kwanza na cha pili sambamba na kifungu namba 131 kifungu kidogo cha kwanza na cha tatu.
Akitoa ushahidi mahakamani hapo Shahidi namba moja ambaye ni babu wa mtoto ameeleza kuwa siku ya tukio mtuhumiwa aliomba mtu wa kuondoka kwenda Naye kutengeneza dawa ya kutoa Ndagu, ndiyo akapatiwa binti ambaye aliambatana Naye baada ya kufika msituni alimlazisha kuuvua Nguo za ndani, binti alipo kataa mtuhumiwa huyo alimkamata kwa nguvu na kisha kumbaka.
Shahidi namba mbili ambaye ni daktari wa hospitali ya Wilaya ya Kishapu ameithibitishia mahakama kuwa mtoto huyo alifanyiwa vipimo na kukuta na michubuko iliyothibitisha kuwa aliingiliwa na mwanaume.
Ushahidi mwingine umetolewa na Askari polisi kupitia fomu ya polisi namba tatu pamoja na maelezo ya onyo yaliyotolewa na mshtakiwa mwenyewe ambaye alikiri kutenda kosa hilo.
baada ya kusikiliza mashahidi hao Hakimu mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Kishapu, Johanitha Rwehabula amesema mahakama imeridhishwa na ushahidi hivyo mtuhumiwa amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela.
Aidha, Hakimu Rwehabula ametoa wito kwa jamii kuachana na vitendo vya ukatili kwa watoto na wanawake kwa jumla kwa sababu hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Katika hatua nyingine Afisa Ustawi wa Jamii anayeshugulikia maswala ya watoto, Rehema Kasita amelaani kitendo hicho cha ubakaji na ameiomba jamii kushirikiana ili kukomesha vitendo hivyo vya kikatili dhidi ya watoto.
"Na laani kitendo hiki cha ubakaji kitendo hiki ni cha kikatili sana dhidi ya watoto ni vitendo vya Kishetani, kwa yeyote anayefanya vitendo kama hivi, aache mara moja, niwaombe pia wananchi kuweni makini na hawa waganga wa Kienyeji kwani wamekuwa ni chanzo cha ukatili kwa watoto, tushirikiane kwa pamoja katika kukomesha vitendo hivi.” Alisema Rehema.
Naye, Mkuu wa dawati la jinsia Wilaya ya Kishapu, Rose Ranton Bwambo ameridhishwa na uamuzi uliotolewa na mahakama ili iwe fundisho kwa watu wengine.