MFANYABIASHARA maarufu wa madini ya Tanzanite jijini Arusha, Pendael Mollel na wenzake watatu, wamekamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumteka mlinzi, kumpiga na kumuua Aprili 19 mwaka huu.
Kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo na wenzake watatu kumethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Justin Masejo na kueleza kuwa mtuhumiwa alikamatwa Moshi alikokimbilia kujificha bà ada ya mauaji hayo.
Masejo amesema leo kuwa watuhumiwa wote wako rumande Kituo Kikuu cha Polisi Arusha, kwa mahojiano na kuna watuhumiwa wengine wanatafutwa, ili kuunganishwa kwenye tukio hilo.
Amesema kwa sasa hawezi kuzungumza kwa undani, zaidi ya kujua kuwa watuhumiwa wako rumande, ila baada ya siku moja ama mbili wahusika wakikamilisha kutoa maelezo na wengine kukamatwa atatoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya tukio zima.
‘’Ninachoweza kusema kwa sasa ni kukiri kuwa mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite, Pendael Mollel, tumemkamata Moshi kwa tuhuma za mauaji, wenzake watatu wamekamatwa Arusha,” amesema Kamanda Masejo.
Habari kutoka vyanzo mbalimbali eneo la tukio Burka karibu na Uwanja wa Ndege wa Arusha, zilidai kuwa tukio hilo la mauaji lilitokea Aprill 19 mwaka huu majira ya saa 1:45 usiku, ambapo Mollel akiwa na wapambe wake walienda kumchukua Stephen Jimmy (43) kwenye nyumba aliyokuwa akilinda, inayomilikiwa na Mtanzania mwenye asili ya Kisomali, Mahmudu Mohamed.
Source: Habari Leo