Breaking

Monday, 25 April 2022

MAMA AMZIKA MWANAE USIKU WA MANANE BAADA YA KUFARIKI KWA NJAA





Salah Jackson (5) mwenye ulemavu wa viungo, mkazi wa kijiji cha Makiwaru Mkoani Kilimanjaro amefariki dunia kutokana na njaa na kisha mama yake mzazi kumzika kimyakimya usiku wa manane.

Mtoto huyo anadaiwa kuzikwa na mama yake mzazi aitwaye Rebecca Siowi (30) usiku wa kuamkia Aprili 22, 2022 nyumbani kwa bibi yake walikokuwa wakiishi yeye pamoja na mama yake baada ya mume kumtelekeza na watoto watano.

Tukio hilo liligundulika baada ya mtoto huyo kutoonekana jioni ya Aprili 21 nyumbani alikokuwa akiishi kwa bibi yake, ambapo bibi yake huyo alifanya jitihada za kumtafuta mjukuu wake huyo bila mafanikio ndipo Aprili 22 alipobainika kuwa amezikwa.

Akizungumzia tukio hilo leo Aprili 23, 2022 Kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amekiri kuwepo kwa tukio hilo, akisema baada ya kupata taarifa ya tukio hilo kutoka kwa wananchi walifika eneo la tukio kuona sehemu alipozikwa mtoto huyo.

Kamanda Maigwa amesema walipofika eneo la tukio walilazimika kuomba kibali cha kuufukua mwili wa mtoto huyo ili kujua sasababu hasa za kifo cha mtoto huyo kutokana na maneneo ambayo yalikuwa yakisemwa mtaani.

"Hili tukio kweli lipo na baada ya Jeshi la polisi kupata taarifa juu ya tukio hilo tulienda kuomba kibali cha kufukua mwili wa mtoto ili kujiridhisha sababu za kifo cha mtoto huyo ni nini kutokana na maneno mengi yaliyokuwepo mtaani.

"Tulifukua mwili jana na kuupeleka hospitali kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na majibu ya daktari yalipotoka yalionyesha kwamba huyu mtoto alikufa kutokana na njaa,” amesema Kamanda Maigwa

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Makiwaru, Barakaeli Nasari alisema alipata taarifa kutoka kwa bibi wa mtoto huyo kuwa mjukuu wake haonekani na ndipo baadaye ilibainika kuwa amezikwa na mama yake bila kuambiwa.

Akizungumzia tukio hilo, jirani wa familia hiyo, Maria Nko amesema hata kama mtoto huyo alikufa kwa njaa mama yake huyo hakupaswa kumzika mwanaye kama mbwa tena usiku wa manane.

"Kwa kweli hili tukio linaumiza na inaonekana huyu mama alikuwa akimtesa huyu mtoto kutokana na ulemavu aliokuwa nao, inakuwaje hao watoto wake wengine hawajafa na
njaa na kwa nini amzike mwenyewe tena?” amehoji.




Source: Mwananchi
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages