
Na Mwandishi Wetu-Moshi
Baraza la Madiwani Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro limemuondoa madarakani Meya wa Manispaa hiyo, Juma Raibu kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo matumizi mabaya ya madaraka.
Raibu ameng’olewa leo Jumatatu, tarehe 11 Aprili 2022 katika kikao cha baraza hilo ambapo kati ya madiwani 28 waliopiga kura, zilizomkataa 18 sawa na asilimia 64.3 na 10 zikiwa upande wake sawa na asilimia 35.7.
Mara baada ya kumaliza kupiga kura na matokeo kutangazwa na naibu meya, Stuart Nkinda atakuwa akikaimu nafasi ya meya hadi baadaye, baraza liliahirishwa.
Akisoma taarifa ya timu ya uchunguzi ya Mkoa, Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Rashidi Gembe amesema Raibu anakabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwamo kutumia nafasi yake vibaya, kupokea rushwa na kuruhusu ujenzi holela katika eneo la CBD, mienendo mibaya na ukosefu wa adabu dhidi ya madiwani wenzake.
Raibu pia anatuhumiwa kutoa maneno ya kuwatambia madiwani wenzake kuwa yeye ni mteule wa kamati kuu ya CCM Taifa na si ngazi ya wilaya wala mkoa, kuchelewa vikao na kutokaimisha vikao kwa naibu meye hata akiwa nje ya ofisi na vikao vingine kulazimisha kuahirishwa kwa kuwa yeye hayupo na kwamba timu hiyo pia imebaini mwenendo mbaya wa Meya huyo.
Tuhuma zingine ni, kuhamisha fedha kutoka kituo cha afya Kaloni na kupeleka Pasua bila kufuata za vikao pamoja na kutuhumiwa kula rushwa na kuruhusu ujenzi holela katikati ya mji.
Pia anatuhumiwa kutumia nafasi yake vibaya na kwenda kushiriki sherehe ya kijana anayedaiwa kuwa na mahusiano ya mapenzi ya jinsia moja ‘mashoga.’
Sherehe hiyo ya siku ya kuzaliwa ya moja ya shoga, ilifanyika tarehe 11 Februari 2022 katika ukumbi wa klabu moja iliyopo kata ya Bondeni, Manispaa ya Moshi ambako Juma alihudhuria kama mgeni rasmi.
Inaelezwa shoga huyo aliyekuwa na wenzake, waliamua kumualika Raibu ili kada hiyo ya watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja, iweze kutambulika kwani wanapata taabu kutambuliwa na mamlaka za serikali.
Kitendo hicho kiliwakwaza watu mbalimbali wakiwemo Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Mkoa waKilimanjaro waliokiandikia barua Chama Cha Mapinduzi (CCM), kulaani tukio hilo na kutaka hatua madhubuti zichukuliwe dhidi ya kiongozi huyo.
Mbali na Bakwata, ndani ya Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, zilidai kuwa kitendo hicho kimewakasilisha madiwani wengi wa CCM na kumtaka kujiuzulu ili kulinda heshima ya chama chake pamoja na Baraza zima la Madiwani.
Raibu aliondoka katika viwanja vya manispaa kwa usafiri wa bodaboda huku wananchi waliokuwemo wakishangilia.
Tayari kamati za siasa za wilaya na mkoa wa Kilimanjaro ulimhoji na kumjadili na kupeleka mapendekezo makao makuu ya kutaka achukuliwe hatua ikiwemo kuvuliwa umeya na kuwekwa chini ya uangalizi wa kiezi 12 kutokana na kitendo hicho walichodai kimekidhalilisha.
Baadhi ya madiwani wa Manispaa hiyo wamesema wamefanya maamuzi ya kihistoria ya kumuondoa Meya madarakani kwa sababu ya matendo yake na tuhuma zinazomkabili.