
Jamii imeaswa kufanya mazoezi ili kujikinga na magonjwa mbalimbali yasiyo ambukiza.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilemela Mhe Said Kitinga wakati wa mbio za kilomita 16 kutoka uwanja wa CCM Kirumba kupitia Pasiansi kuelekea Ilemela Redio Free na kisha kurudi CCM Kirumba ikishirikisha vilabu vya mbio vinavyopatikana mkoa wa Mwanza.

Kitinga amewataka wananchi kujitokeza katika mazoezi kwani mbali na kuimarisha afya yamekuwa chachu katika kuleta umoja, upendo na mshikamano
"Tukishiriki mazoezi tunajikinga na magonjwa yasiyo ambukiza lakini pia tunaimarisha umoja wetu na mshikamano hata katika shughuli za maendeleo si mnaona hapa tupo klabu mbalimbali" amesema Kitinga
Aidha Kitinga ameviasa vilabu vilivyoshiriki mbio hizo kuendelea na mbio binafsi Kila mara wanapopata nafasi badala ya kusubiria mbio za mara Moja zinazokutanisha vilabu vyote vya Mkoa zinazoratibiwa na ofisi ya Mkuu wa wilaya hiyo Mhe Hassan Elias Masalla
Kwa upande wake Kaimu Afisa Michezo wa wilaya ya Ilemela Ndugu Kizito Bahati mbali na kumshukuru Katibu Tawala Kwa kuongoza mbio hizo akaongeza kuwa mbio hizo ni Utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kasim Majaliwa Majaliwa hivi karibuni wakati wa kikao chake na maafisa michezo wote nchini.
Peter Julius ni moja ya mwananchi aliyeshiriki mbio hizo ambapo amempongeza Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masalla Kwa kuasisi mbio hizo huku akiwaasa wananchi wenzake kuendelea kuiunga mkono Serikali katika shughuli mbalimbali za kijamii inayozianzisha ikiwemo michezo.