Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza imeibuka kidedea katika tuzo za usimamizi bora wa miradi ya afya na elimu zilizotolewa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel kwa wilaya zote za mkoa huo.
Wilaya hiyo imefanikiwa kutwaa tuzo ya usimamizi bora wa miradi ya afya kwa kuwa mshindi wa kwanza, tuzo ya mshindi wa pili mitihani ya kidato cha pili kitaifa kwa mwaka 2021, tuzo ya mshindi wa kwanza mitihani ya kitaifa kwa darasa la nne kwa mwaka 2021.
Katika hafla hiyo mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel amezitaka halmashauri zote za mkoa huo kuweka msukumo katika kuongeza kasi ya usimamizi wa miradi ya maendeleo Kwa wananchi pamoja na matumizi sahihi ya fedha za miradi ya maendeleo zinazotolewa na Serikali.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Ilemela, Hassan Masalla ameshukuru Kwa wilaya yake kufanikiwa kutwa tuzo hizo huku akiahidi kuongeza kasi katika kuisimamia wilaya yake katika kutekeleza miradi yenye tija Kwa wananchi itakayozingatia mahitaji ya wakati na thamani ya fedha.
Zoezi la utoaji wa tuzo hizo lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka wilaya zote za mkoa wa Mwanza wakiwepo wakuu wa wilaya, wakurugenzi, mameya na wenyeviti wa halmashauri.