Na Mwandishi Wetu, Geita
HOSPITALI ya rufaa ya kanda Chato, imeanza kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo ili kuwapunguzia wananchi gharama na muda wa kwenda hospitali ya Jakaya Kikwete jijini Dar es Salaam.
Mbali na huduma za kibingwa, inatarajia kufundisha wataalam wa fani za Udaktari na uuguzi sambamba na kufanya utafiti wa magonjwa ya Binadamu.
Ofisa utumishi wa hospitali hiyo, Elly Aketch, amebainisha hayo akieleza kuwa wameanza kwa mafanikio makubwa kutokana na baadhi ya wagonjwa kupatiwa huduma za kibingwa na zile za kawaida na kwamba hatua hiyo imewasaidia wananchi kutumia gharama kidogo ikilinganishwa na iwapo wangesafiri kwenda hospitali ya Jakaya Kikwete.
"Tunatarajia kutoa huduma bora zaidi ikiwezekana kuzidi hata zinazotolewa pale hospitali ya moyo ya Jakaya Kikwete...tunaamini hospitali hii itakuwa mkombozi kwa wananchi waliopo ukanda wa ziwa"amesema.
Licha ya kwamba ujenzi wa baadhi ya majengo ya kulaza wagonjwa unaendelea ikiwemo jengo la huduma za mama na mtoto, pia huduma zinazidi kuimalika ambapo wagonjwa kutoka mkoa wa kagera na Geita wamepatiwa huduma na kupona.
Aketch, amedai kwamba ujenzi wa hospitali hiyo umefanyika kwa awamu tatu ukitanguliwa na majengo ya wagonjwa wa nje,dharura, maabara, dawa na wagonjwa mahututi ambayo yamekamilika.
Huku awamu ya pili ikiwa imehusisha jengo la mama na mtoto lenye vyumba 250 ambalo linakadiliwa kuchukua wagonjwa 500 kwa wakati mmoja pamoja na jengo la mionzi.
Kadhalika awamu ya tatu itahusisha jengo kubwa la ghorofa 9 ambalo litakuwa na huduma mbalimbali na kwamba litaondoa uhaba wa majengo ya kutolea huduma kwa jamii.
Baadhi ya wakazi wa mji wa Chato, Didas Kabantega na Imelda Adamu, wameishukuru serikali kwa uamuzi wake wa kusogeza huduma za kibingwa maeneo yao kwa madai kwamba awali wagonjwa wengi walikuwa wakipoteza maisha kutokana na huduma hizo kupatikana mbali.