Breaking

Tuesday, 5 April 2022

EWURA YATANGAZA BEI MPYA ZA MAFUTA..PETROL YAPANDA KWA TSH 321



Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetoa Bei Mpya ya Mafuta kwa Tanzania ambayo itaanza rasmi kutumika kesho Aprili 06, 2022.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Jumanne Aprili 5, 2022 Mkurugenzi wa Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Gerald Maganga amesema kuanzia kesho Jumatano, Aprili 6,2022 bei mpya ya petrol kwa mafuta yanayopokelewa kupitia Bandari ya Dar es salaam itakuwa Sh2,861 kutoka Sh 2,540 ikiwa ni ongezeko la Sh321.


Kwa upande wa dizeli bei mpya itakuwa Sh2,692 kutoka Sh2,403 ya sasa ikiwa ni ongezeko la Sh289. Bei ya mafuta ya taa itapanda kutoka Sh2,208 hadi Sh2,682 ikiwa ni wastani wa Sh474.

Maganga amesema mafuta ambayo yatapitia Bandari ya Tanga, bei ya petrol itakuwa Sh2,848 kutoka Sh2,563 ikiwa ni ongezeko la Sh285.


Kwa upande wa dizeli bei itaongezeka kutoka Sh2,484 hadi Sh2,779 ikiwa ni ongezeko la Sh295 kwa lita moja.


Mafuta ambayo yatapokewa kupitia Bandari ya Mtwara bei ya petrol kwa lita moja itakuwa Sh2,678 kutoka Sh2,577 ikiwa ni ongezeko la Sh100.


Bei ya dizeli kwa lita moja itakuwa Sh2,811 kutoka Sh2,530 ikiwa ongezeko la Sh281.


Hata hivyo, Maganga amesema kuwa bei hizo zimejumuisha tozo ya Sh100 ambayo Serikali ilitangaza kuiondoa mwezi Machi, 2022 kabla ya Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza kuirejesha akisema utaribu wa kuindoa haukufuatwa kwa kuwa fedha hiyo ilishapangiwa bajeti.

Aidha, Maganga amefafanua kuwa Kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani ili mradi bei hizo zisivuke bei kikomo au kushuka chini ya bei iliyoruhusiwa kama ilivyokokotolewa Kwa kutumia formula na kanuni za EWURA zinazopanga Bei za mafuta za mwaka 2022 zilizotangazwa kupitia gazeti la Serikali namba.57 la tarehe 28Januari mwaka huu.


Bei ya nishati hiyo inapanda wakati wananchi wakilalamika kupaa kwa bei za bidhaa mbalimbali za vyakula hasa wakati huu wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani.


Vita ya Urusi na Ukraine ambayo imedumu kwa zaidi ya mwezi sasa imetajwa kuwa sababu ya kupanda kwa bei ya nishati hiyo kwenye soko la dunia.


Hata hivyo Russia ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages