Breaking

Friday, 22 April 2022

DKT MABULA ATOA SADAKA YA FUTARI KWA TAASISI ZA ELIMU JIMBO LA ILEMELA





Mbunge wa Jimbo la Ilemela Na Waziri wa Ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi Dkt Angeline Mabula amekabidhi sadaka ya futari Kwa taasisi za Elimu zilizopo katika jimbo la Ilemela ili kuwawezesha wanafunzi waislamu waweze kufuturu katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan.


Taasisi za elimu zilizopata sadaka hizo ni Chuo Cha Mipango, shule ya sekondari Bwiru wasichana na shule ya sekondari Bwiru wavulana ambapo ametoa kwa kila taasisi Sukari Kilo 110, Mchele Kilo 110, Tambi na Tende.



Akizungumza wakati wa makabidhiano yaliyofanyika April 21, 2022 Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Kazungu Idebe amesema kuwa Mbunge wa Jimbo hilo amekuwa na utaratibu wa kuungana na waumini wa dini ya kiislamu unapofika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan kila mwaka kwa kutoa sadaka ya futari ili kusaidia waumini hao waweze kufunga kwa salama na amani.


"Mhe Mbunge alitamani kuwepo yeye mwenyewe katika zoezi hili, Lakini kutokana na majukumu ya kitaifa aliyopewa ameshindwa ingawa siku za hivi karibu alianzisha yeye mwenyewe zoezi hili Kwa kutoa sadaka hii katika vituo vya watoto yatima, Wajane, Misikiti, Wazee na Watu wenye uhitaji, Na leo sisi wasaidizi wake akaamua tumuwakilishe kuendelea alipoishia." Amesema



Kazungu amewaasa wanafunzi hao kutumia mwezi huu mtukufu kuombea taifa na viongozi wake wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan huku akisisitiza kuwa taifa lolote lenye hofu ya Mungu lazima liwe na Maendeleo.


Kwa upande wake Mkuu wa shule ya Sekondari ya wasichana Bwiru, Mwalimu Mektilda Shija ametoa shukran kwa Mbunge kwa kuendelea kutoa ushirikiano wa mara kwa mara kwa shule hiyo.


"Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Mabula amekuwa mtu wa msaada katika shule hii, na si mara ya kwanza kufika kutoa misaada, mara kadhaa amekuwa akishirikiana nasi katika kutatua kero mbalimbali zinazotukabili" Amesema



Naye Mwanafunzi wa kidato Cha Tano anaesoma masomo ya mchepuo wa sayansi (CBG) katika shule ya wasichana Bwiru, Hawa Japhari amemshukuru Mbunge Dkt Angeline Mabula Kwa msaada alioutoa.



Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages