Breaking

Wednesday, 20 April 2022

DC MASALA ATOA MAAGIZO USIMAMIZI UJENZI WA MIRADI YA MAENDELEO ILEMELA





Mkuu wa wilaya ya Ilemela Hassan Masala ameridhishwa na kupongeza hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa shule ya sekondari kata ya Buzuruga itakayogharimu kiasi cha shilingi milioni mia nne na sabini mpaka kukamilika kwake.


Dc Masala amebainisha hayo leo Jumatano April 20, 2022 wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya wilaya hiyo akiwa ameambatana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama, wataalam wa manispaa na baadhi ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).


Miradi iliyotembelewa ni pamoja na ujenzi wa hospitali ya wilaya utakaogharimu kiasi cha shilingi milioni mia nane, ujenzi wa kituo cha afya Kayenze wenye kiasi cha shilingi milioni mia tano, na ujenzi wa shule mpya ya sekondari Buzuruga.


Akizungumza wakati akikagua miradi hiyo DC Masala amewataka wananchi, wataalam na viongozi wa maeneo inapotekelezwa miradi hiyo kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati ikizingatia ubora unaotakiwa kwa gharama nafuu zilizopangwa.


"Tumetembelea miradi ya maendeleo kukagua nini kinaendelea, na tutaendelea kufanya hivyo kadri tunapopata nafasi, Naridhishwa na kasi ya ujenzi wa hapa Buzuruga kikubwa tuzidi kujitahidi ili mradi huu ukamilike kwa wakati " Amesema



Amewataka mafundi waliokabidhiwa jukumu la ujenzi kuhakikisha hakuna ubadhirifu wowote utakaojitokeza huku akiwaasa wajumbe wa kamati za ujenzi kuwa makini katika usimamizi wa vifaa vya ujenzi kwa kuwa Serikali haitavumilia ubadhirifu wowote utakaojitokeza.

Aidha amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hasan kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Joseph Apolinary amewahakikishia wananchi kuwa fedha ya utekelezaji wa miradi hiyo ipo kikubwa ni mafundi kuongeza kasi ya ujenzi ili kwenda sambamba na kalenda ya bajeti ya Serikali kuepuka kurudishwa kwa fedha hizo Serikali kuu.



Crydon Gondwe ni miongoni mwa wajumbe wa kamati wanaosimamia ujenzi wa shule ya sekondari Buzuruga ambapo ameshukuru viongozi hao kutemebelea mradi huku akiahidi ushirikiano kwa niaba ya wananchi wengine.

Kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Ilemela itaendelea na ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya wilaya hiyo wiki ijayo kwa kutembelea miradi ya barabara na mengineyo kadri ya itakavyopangwa.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages