Breaking

Monday, 11 April 2022

"ASILIMIA 1.4 YA WATANZANIA WANAJISAIDIA VICHAKANI" WAZIRI UMMY





Na Mwandishi Wetu-Dar es Salaam


Imeelezwa kuwa tangu kampeni ya nyumba ni choo izunduliwe mwaka 2017, imeleta matokeo chanya kwa wananchi kujenga vyoo bora na kuondokana na kujisaidia vichakani au vyoo ambavyo havistahili.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu April 11, 2022 jijini Dar Es Salaam na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati wa hafla ya miaka mitano ya utekelezaji wa kampeni ya Usichukulie poa Nyumba ni Choo.

Waziri Ummy amesema tangu kampeni hiyo iliyozinduliwa na aliyekuwa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan (ambaye kwa sasa ni Rais wa Tanzania) ilikua na lengo la kuhamasisha kila kaya kuwa na choo bora hadi kufikia asilimia 75 ya kaya zote nchini ifikapo Juni 2021.

Kampeni hiyo imeleta matokeo ambapo idadi ya kaya zenye vyoo bora imeongezeka hadi kufikia asilimia 72.1 kutoka asilimia 37.1 mwezi Desemba 2017 huku kujisaidia ovyo vichakani kumeweza kupungua kutoka asilimia 5.7 hadi kufikia asilimia 1.4.

“Ukiangalia katika kila kaya 100, kaya 72 zina vyoo bora lakini shirika la afya duniani (WHO) pamoja na UN wamesema lengo ni kuwa na asilimia 100 ambapo kila kaya, taasisi au sehemu zote zinazotumiwa na watu zinatakiwa kuwa na choo bora”

Waziri Ummy amesema bado kuna tatizo la kutokua na vyoo bora katika shule nyingi nchini hivyo Wizara imejipanga kuzindua kampeni hiyo awamu ya pili ili kuhakikisha inafanya uhamasishaji kwa Viongozi na watendaji wa halmashauri kuhakikisha wanajenga vyoo bora pamoja na vifaa vya kunawa mikono.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages