Breaking

Friday, 22 April 2022

AMUUA MFANYAKAZI WA NDANI NA KISHA KUJARIBU KUJIUA KWA SUMU


KIJANA ambaye alikuwa mfanyakazi wa kulisha ng'ombe amemuua msichana wa kazi za ndani kwenye nyumba waliyokuwa wakifanya kazi pamoja huku chanzo kikiwa bado hakijafahamika.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, ACP Pius Lutumo amesema kuwa, mtuhumiwa na marehemu walikuwa wakifanya kazi kwa mtu aliyefahamika kwa jina moja la Samwel.


Amesema kuwa, mtuhumiwa ambaye jina limehifadhiwa kwa sababu za kiuchunguzi umri wa miaka 27 alimuua Dawiya Mshihiri (30) kwa kumshambulia na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili.


"Mtuhumiwa baada ya tukio hilo alijaribu kujiua kwa kunywa sumu, lakini hakufanikiwa na kukamatwa na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Tumbi kwa matibabu akiwa chini ya ulinzi wa polisi,"amesema Lutumo.


Aidha, amesema kuwa mtuhumiwa na marehemu walikuwa wakifanya kazi kwenye nyumba moja na Polisi wanaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo.


Amebainisha kuwa, mara upelelezi utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria na anawasihi wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi.
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages