Severine Mbullu, Lango la habari- Kishapu
Mahakama ya wilaya Kishapu Mkoani Shinyanga imemhukumu kifungo cha maisha Jela Tine Christopher Mbembele (51) kwa kosa la kumlawiti mtoto mwenye umri wa miaka Saba (7).
Mbembele amehukumiwa kifungo hicho leo Jumatano April 27, 2022 baada ya mahakama kujiridhisha na kumkuta na hatia ya kumlawiti mtoto huyo.
Katika shauri namba 54 la mwaka 2021 lililowasilishwa na mwendesha mashtaka wa serikali Masenza Magunila Mbele ya Hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya Kishapu Amada Ismail Mshtakiwa anadaiwa kufanya kosala la kulawiti mtoto huyo mnamo Juni 15, 2021 katika kijiji cha Maganzo katika halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga.
Magunila amesema kuwa kosa hilo ni kinyume na kifungu cha sheria namba 154 kifungu kidogo cha kwanza na cha pili sambamba na kifungu namba 2 kifungu kidogo cha kwanza na cha tatu kosa.
Kwa upande wake Hakimu Amada Ismail amesema kuwa mahakama imezingatia ushahidi wa fomu ya polisi namba 3 uliotolewa na shahidi namba mbili ambaye ni daktari katika Hospitali ya Kolandoto aliyeithibitishia mahakama kuwa alipompima mtoto huyo alikuta michubuko na kueleza kuwa aliingiliwa na mwanaume nyuma ya maumbile.
Mahakama imemtia hatiani mshtakiwa baada ya kusililiza mashahidi wanne akiwemo Bibi wa mtoto, Daktari wa Hospitali ya Kolandoto, mtoto wa mshatakiwa pamoja na askari polisi.
Uthibitisho mwingine umetolewa kwenye Taarifa ya uchunguzi wa kijamii wa awali kutoka kwa Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Kishapu ukithibitisha Tukio la mtoto huyo kulawitiwa.
Baada ya mahakama kusililiza pande zote za ushahidi pamoja na kuthibitishiwa na vielelezo viwili kikiwemo cha fomu ya polisi namba tatu pamoja na maelezo ya onyo yaliyotolewa na mshtakiwa mwenyewe ambaye alikiri kutenda kosa hilo kwa shahidi namba nne ambaye ni askari polisi.
Hakimu Amada Ismail amesema baada ya kuzingatia sheria iliyomtia hatiani mshitakiwa kwa kosa la kumlawiti binti mwenye umri chini ya miaka kumi adhabu yake ni kifungo cha maisha na hivyo mahakama imemuhukumu Tine Christopher Mbembele kifungo cha maisha jela.