Mahakama ya Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga imemuhukumu kifungo cha maisha jela Baraka Andrea (26) mwalimu wa Tuition baada ya kukutwa na hatia ya kulawiti watoto watatu wa shule ya Msingi Majengo wenye umri chini ya miaka 10.
Akisoma hukumu hiyo leo Jumatatu April 25, 2022 mbele ya Mahakama hiyo Hakimu Donasian Agustino amesema Mahakama inamhukumu mshtakiwa kwa mujibu wa kifungu namba 154(a) na 2 sheria kanuni ya adhabu.
Amesema baada ya kupitia ushahidi uliotolewa mahakamani umejitosheleza bila kuacha shaka hivyo Mahakama inamtia hatiani mshitakiwa huyo kwa kosa hilo la ulawiti.
Kabla ya Hakimu kusoma hukumu hiyo, mwendesha mashitaka Satuninus Kamala aliiomba mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.
Kwa upande wake mshitakiwa Baraka Andrea ameomba kupunguziwa adhabu kwani ana familia inayomtegemea.
Hata hivyo mbali na mshtakiwa kuomba kupunguziwa adhabu tayrai mshtakiwa alikuwa anatumikia kifungo cha maisha gerezani kwa kesi nyingine ya kulawiti hivyo mahakama imetupilia mbali ombi hilo.