Breaking

Monday, 7 March 2022

WAZIRI UMMY ATOA TAHADHARI JUU YA MATUMIZI YA P2


Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ametoa tahadhari juu ya matumizi holela ya vidonge vya dharura vya kuzuia mimba (P2).

Ameyasema hayo leo Jumatatu Machi 07, 2022 wakati akiongea kwenye kipindi cha Good Morning kinachorushwa na Wasafi FM ikiwa ni sehemu ya vipindi maalum kuelekea siku ya wanawake duniani.

Waziri ummy  ameeleza kuwa matumizi holela na ya mara kwa mara  yana madhara kwa Afya ya mwanamke kwa kumuweka katika hatari ya kupata Ugumba na Saratani.

"Vidonge hivi vya P2 sio vya kunywa kila siku, tutaendelea kutoa elimu ya afya ya uzazi ili jamii iweze kuelewa pia tutaendelea kuweka fedha kwenye masuala ya Afya ya uzazi, mama na mtoto". Amesema Waziri Ummy.

Ametoa wito kwa wazazi na walezi kutoa elimu kwa watoto wao juu ya afya na mabadiliko ya mwili ikiwemo vichocheo vya hisia bila kuona aibu.

Aidha amesema Wasichana wa sasa hasa wa vyuoni wanaogopa kupata mimba kuliko kupata Ukimwi jambo ambalo ni hatari kwa afya zao kwani wanajiweka katika hatari ya kupata magonjwa ya kuambukizwa.


"Usipomueleza mtoto vizuri masuala ya Afya yake, mwili wake ataenda kuyapata kwenye njia ambazo sio sawa kama kwenye mitandao ya kijamii na kwa marafiki wanaozunguka jambo ambalo linamuweka kwenye hatari ya kupata maambukizi". Amesema Mhe. Ummy.


Waziri Ummy amesema ili kutumia vizuri njia za uzazi wa mpango za Kisasa unatakiwa kwenda kwa daktari kujua hali na kupata ushauri na kuendelea kusisitiza matumizi ya njia za asili kama kuangalia kalenda ambayo kwa sasa unaweza kutumia hata simu janja ya mkononi (Smartphone).

Vile vile Waziri Ummy ametoa wito kwa wanawake kuwa na tabia ya kuchunguza afya zao mara kwa mara ili kuepuka magonjwa kama Saratani ya Kizazi na Saratani ya Matiti kwani hivi sasa kati ya wanawake 100 wanaofanyiwa uchunguzi wanawake 40 hupatikana na saratani ya mlango wa kizazi.

Ameitaka jamii kuzingatia mfumo bora wa maisha na kuacha matumizi ya chumvi nyingi, sukari na mafuta mengi wakati wa kuandaa chakula.

-Mwisho-
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages