Breaking

Monday, 21 March 2022

WAZIRI JAFO ATOA UFAFANUZI WA RIPOTI YA MTO MARA, AWATAKA WATANZANIA KUWA WATULIVU

 


Waziri wa Nchi wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema baada ya kupokea taarifa ya Kamati ya Kitaifa iliyochunguza uchafuzi wa mazingira uliojitokeza hivi karibuni ndani ya Mto Mara, ameagiza timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais kushirikiana na Wizara ya Maji na Wizara ya Mifugo kuipitia kwa kina taarifa hiyo na kuwasilisha uchambuzi wa kitaalamu pamoja na Mpango kazi wa utekelezaji.


Ameyasema hayo leo tarehe 21 Machi 2022 jijini Dodoma mara baada ya kukutana na waandishi wa habari na kutoa ufafanuzi kuhusu ripoti iliyowasilishwa kwake na Kamati ya Kitaifa iliyochunguza uchafuzi wa mazingira mwishoni mwa wiki.


Amewataka watanzania kuwa watulivu na kuepusha taharuki inayoendelea mitandaoni kwani azma ya Serikali ni kulinda afya ya wananchi wake.  Pia, ameagiza ripoti hiyo ya wataalamu itafsiriwe kwa lugha ya Kiswahili na kusambazwa kwa umma ili maudhui yake yaweze kufahamika kwa jamii.


SomaKINYESI CHA MIFUGO CHANZO CHA KUFA SAMAKI MTO MARA - KAMATI

Kuhusu taarifa ya awali ya uchunguzi wa kimaabara iliyotolewa na Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, Dkt. Jafo amesema taarifa hiyo ndio ilipelekea kuundwa kwa Kamati ya kuchunguza kwa kina chanzo cha uwepo wa kiwango cha mafuta na kukosekana kwa hewa ya oksijeni, ambapo imebainika kuwa taarifa hiyo haikinzani na ile ya Timu ya Kitaifa


Aidha, Dkt. Jafo amesema anakaribisha na kupokea ushauri na maoni mbalimbali kutoka kwa wadau na wataalamu wa mazingira wa namna bora ya kutatua changamoto za mazingira nchini.

 

Machi 12, 2022 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo aliunda Kamati ya Kitaifa yenye wajumbe 11 kuchunguza chanzo cha uchafuzi wa mazingira uliojitokeza ndani ya Mto Mara chini ya uenyekiti wa Prof. Samwel Manyele wa Idara ya Uhandisi wa Kemikali na Madini kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kamati iliyowasilisha taarifa yake 19 Machi 2022.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages