Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa ametoa wito kwa Mameya wa Majiji na Manispaa kutangaza na kutumia vizuri fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana katika maeneo yao.
Ameyasema hayo leo Ijumaa Machi 25, 2022 Jijini Dodoma wakati akifungua kikao kilichowakutanisha Mameya wa Majiji, Manispaa na shirika la Big Phlanthropy ili kujadili masuala ya maendeleo na fursa za uwekezaji zinazopatikana katika maeneo yao.
“Baada ya kuona taswira ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hasssan ya kukaribisha uwekezaji na kutangaza fursa zilipo Tanzania, tumekutana katika kikao hiki kujadili namna ya kutumia vizuri fursa zilizopo katika Majiji na Manispaa mnazotoka” amesema Bashungwa
Waziri Bashungwa ameeleza kuwa katika Miji na Majiji kuna ongezeko kubwa la wananchi hasa vijana wanaojishughulisha na uzalishaji wa bidhaa ambazo zipaswa kuongezewa thamani kabla ya kupelekwa sokoni ambayo ni fursa inayopaswa kuwekewa mkazo ili kutoa ajira kwa wananchi.
Amefafanua kuwa ili kuleta ushindani wa bidhaa katika soko la kimataifa inapaswa bidhaa zote zinazozalishwa ziongezewe thamani kuanzia zinapozalishaji hadi ufungashaji ili ziweke kuvutia na kuleta ushindani katika soko la kimataifa.
Aidha, Waziri Bashungwa amewataka Mameya hao kuhakikisha wanaeleza mafanikio yanayoletwa na Serikali katika maeneo yao na kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo inayoendelea kutekezwa.
Wakati wakichangia hoja Mameya hao, Wameeleza kuwa katika maeneo yao kuna fursa nyingi ambazo zinahitaji kuendelelezwa japokuwa kuna ukosefu wa elimu ya uwekezaji kwa kutumia teknologia katika sekta mbalimbali hasa kilimo na biashara.