Breaking

Thursday, 31 March 2022

WATUMISHI WA UMMA WANAOFANYA KAZI KWA MAZOEA WAONDOLEWE TUAJIRI WENGINE - WAZIRI BASHUNGWA



Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa amesema hatawafumbia macho watumishi ambao hawatoshi na kuwa wataondolewa kwenye utumishi wa umma na si kuwashusha vyeo au kuwahamisha.


Mhe. Bashungwa ametoa wito huo Machi 30, 2022 alipozungumza  na waandishi wa habari Jijini Dodoma muda mfupi baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kuiagiza Ofisi ya Rais  TAMISEMI kuzisimamia Halmashauri ipasavyo na kuchukua hatua kwa watumishi wenye matumizi mabaya ya fedha za Serikali.


Amesema kumekuwepo na utaratibu wa kuwashusha vyeo watumishi wachache ambao wanafanya kazi kwa mazoea na kutozingatia taratibu za kiutumishi lakini chini ya usimamizi wangu hilo jambo halivumiliki watatolewa kwenye utumishi wa umma maana wanadhohofisha mchakato mzima wa kuleta maendeleo kwa Watanzania.


“Nimuhakikishie Mheshimiwa Rais kwa maagizo aliyoyatoa leo kuhusu weledi na uadilifu wa Watumishi wa umma, nitaanzia hapa Ofisi ya Rais TAMISEMI kuhakikisha tunajenga taswira na mwelekeo unaoendana na ofisi ya Mheshimiwa Rais” amaesema Bashungwa

Waziri Bashungwa  amewataka  watumishi  katika  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kufanya kazi kwa bidii, kujituma  na uadilifu mkubwa na kwa wachache wanaoenda kinyume na taratibu hizo watachukuliwa hatua kwa kutolewa kwenye utumishi wa umma.


Amesema matarajio yake ni kuona wale wachache waliokuwa wanaenda kinyume wanabadilika na kujirekebisha maana kuna Watanzania wasomi na wazalendo wapo mtaani ambao wakipewa nafasi wataweza kutumikia Watanzania kwa uaminifu.

 

Aidha, Waziri Bashungwa amemwagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI ndani ya siku tatu kuhakikisha anamaliza uchambuzi wa Wawekahazina wa Halmashauri ambao hawafanyi kazi  kikamilifu ili waweze kuchukuliwa hatua. 


Pia, Waziri  Bashungwa amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanasimamia nidhamu ya Utumishi katika maeneo yao hasa katika usimamizi wa fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuchukua hatua mapema kabla ya Wizara haijalazimika kufanya hivyo.

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia langolahabari@gmail.com au WhatsaApp: +255 621 896 990

Pages